SAFARI YA UKOMBOZI

👤 Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira [🇹🇿]

Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

Waefeso 4:12-14

Lengo kubwa la mafundisho haya ili tuweze kukamilishwa na kujengwa ili kufika pale Mungu alipotuandalia pasipo kupoteza mwelekeo wa udanganyifu wa ibilisi. Kuna vitu vitakuja kutoka kwa ibilisi na vitakusukuma huku na kule au kuna watu watakuja na ufahamu wao na kwa kupitia neno la Mungu na watakusukuma na wewe kwa sababu hukumbuki Neno linasema nini unajikuta umeingia mahali ambapo hukutakiwa uingie.

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 2 Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

Kutoka 15:1-2

Mungu anapokupa kitu ambacho hukustahili inabidi umsifu mfano kupata mke au mme ni mpango wa Mungu. Tambua kuwa hata kupata mtoto ni mkono wa Mungu – ina maana kuwa sio kwa nguvu zako bali kwa mkono wa Bwana.  Kuna mambo makuu mawili ambayo tunajifunza hapa:

 1. Kujua kipi katika maisha yako ni mkono wa Mungu na kipi ni nguvu ya Mungu.
 2. Baada ya kugundua peleka shukrani au sifa kama ni wimbo au kwa chochote. Kuna vitu vingine ambavyo ni kwa uwezo wako: mfano kuamka asubuhi sio nguvu zako. Wewe ukiamkaasbuhi sio uwezo wako, wengine akiamka asubuhi anakuwa amekufa au anaumwa, hivyo ni vema kukukumbuka ni nini kinaendelea kwenye maisha yako.

Ni hekima kutambua nini kilitendeka katika maisha yako, kama hutakumbuka Mungu kufanya nini katika maisha yako basi kukua katika Kristo inakuwa ngumu sana. Baada ya pasaka Musa Akawaambia watuwake mambo haya: Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Musa alimwendea Farao akiwa na nguvu ya Mungu, lakini alipoelekea bahari ya Shamu alikuwa na uwepo wa Mungu na palipo na uwepo wa Mungu pana nguvu ya Mungu. Katika uwepo wa Mungu hakuna uchache bali kuna utele lakini hautaweza kuufikia kama haujakua kiroho, kuwepo katika uwepo wa Mungu kunahitaji nidhamu kama hautakumbuka nini kilitokea hataruhusu nguvu yake iende na wewe. Atakupa nguvu zake ili ufukuze mapepo na kuponya wagonjwa lakini si uwepo wake. Mungu anakupa kutumia uwezo ulionao kujenga nyumba, kufukuza mapepo, na kuna vitu ambavyo hutaki kutumia uwezo wako na ndiyo maana Mungu alimwambia Musa gawanya bahari “wakavuka” na walipomaliza adui zao walizama hapo baharini.

Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

Kutoka 15:6

Anazungumzia kuhusu mkono wa Mungu, maana kuna nguvu ya Mungu na mkono wa Mungu. Ukisoma Biblia utabaini kuwa ajabu la kwanza ambalo Musa alifanya ni kuhusu nyoka mpaka pigo la tisa aliamuru Musa, lakini ilipofika pigo la kumi Mungu alifanya mwenyewe lakini ilipofika saa ya kuua alifanya mwenyewe. Katika safari hii ya wokovu hakikisha unapata taarifa za kutosha kuhusu wewe ni nani. Mungu hakutaka wana wa Israeli kuua watu wa Misri kwa sababu hawa Wamisri walikuwa ni wakuu wao, watu ambao waliwalisha chakula, walikuwa wakuu wao. Ndiyo maana Daudi hakutaka kumuua Sauli kwa sababu alikuwa mkuu wao. Ukiona mkuu au kiongozi wako anakutesa usijaribu kumuua hivyo nakushauri ukiona tatizo kwake wewe kimbia tu. Mtu yeyote anayekuwa mkubwa, tambua ameruhusiwa na Mungu. Kiongozi ni kiongozi! Mungu alishawaonya wana Isreli. Hii ni sababu pekee ambayo ilipelekea Mungu asiruhusu wana wa Israeli kuwaua Wamisri. Ukimgusa aliye juu yako humgusi yeye, bali unamgusa Mungu aliye juu yake.

Hatuhitaji kugombana na walioko juu yetu, kama unatamani kutembea na Mungu na kuwa na uwepo wa Mungu sio sifa kubishana na bosi wako. Na wewe kiongozi Mungu akikuinua usiwatese walio chini yako!

Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

Kutoka 15:16

Walikuwa na tabia ya kwenda kuwafuatilia, lakini tunaona hapa sasa akawavusha wa kwake na akawaangaiza adui.

Ni wakati gani hawa watu walinunuliwa? Walinunuliwa walipokuwa wanakula pasaka, kwa tendo la pasaka Musa aliwaambia “Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.

Kutoka 15:17

Siku utakapo kubali kwamba umenunuliwa kwa Damu ya Yesu ndiyo siku ambayo kung’ang’ana kwako kutakoma, je unakubali kwamba umenunuliwa? Kama umenunuliwa lazima utende sawa sawa na mnunuzi (Yesu) ukifanya hivyo atakupa kupanda katika mlima wake na katika urithi wake hivyo unakuwa mrithi, kwa nini unateseka leo? Kwa sababu haujakubali kwamba umenunuliwa. Ukikubali kununuliwa unaingia kwa kutimiza mambo haya matatu: utiifu, uaminifu, kujitoa.

 1. Uaminifu ni Mungu “Mungu ni mwaminifu, hivyo ukiwa unaaminika mbele za Mungu na wanadamu ina maana sasa unamwakilisha Mungu sawasawa”
 2. Utiifu ni Yesu “hivyokatika utii unafanyika mwana wa Mungu”
 3. Kujitoa ni Roho Mtakatifu “hii ni kazi ya roho, kujitoa unapokuwa unajitoa unakuwa unamvutia Roho Mtakatifu”

Hivyo uaminifu wako unaisababisha mbingu ikuamini, hivyo unaweza kupewa kuwa na vingi hata ukuu. Utii utakusababisha ustawi ili ule na kuishi vizuri. Na kujitoa kunakusababisha uwe katika uwepo wa Mungu, uweze kubeba nguvu zake na uwepo wake, na hapo ndipo unaruhusiwa kumwakilisha, unaruhusiwa kubeba karama za roho na unaruhusiwa kuitwa mafuta.

Unapoishia kujitoa unakuwa ni mbegu na sasa unaweza kupandwa! Na sasa unaweza kuitwa heri mtu yule maana umepandwa na sasa unakuwa na urithi wako. Unajikuta si wewe tena.

Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? 25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko.

Kutoka 15:23-25

Safari hii ni safari ya kutoka au safari ya Ukombozi, yaani kutoka kwenye mateso. Utakuwa unakombolewa hatua kwa hatua na siku ukifika sasa utasema nimeipata. Kwa nini watu ambao walikuwa wakimsifu Mungu walianza kunung’unika? Watu walewale walioshangilia kuwa wameanza safari ndiyo walioanza kulalamika, sababu ya kulalamika kwao ilikuwa kwa sababu walisafiri siku tatu bila kukuta maji. Mungu alikuwa akiwafundisha ni jinsi gani ya kupambana na maisha. Kimsingi alitaka wamyumaini Mungu kwa kila kitu. Na utaona hata walipoyakuta maji yalikuwa ni machungu na akawaonesha kwamba kwenye kila tatizo lililoko hapo ulipo lina jawabu hapo hapo ulipo. Ni kweli jambo hilo linaweza kuwa gumu lakini linawezekana. Kilichotokea ni kwamba Mungu aliwapa mti wakanywa maji.

Kilichofuata aliwakemea, kwa sababu walikuwa wanalalamika badala ya kumwambia Musa kuwa tuna kiu ya kunywa maji. Mungu hakuyaponya maji bali Musa ndiye aliyeyaponya, unahitaji kuwa na Mungu ili akujuze jinsi ya kufanya.

Majibu yako hayapo Arusha, Mwanza, Sengerema wala Zanzibar bali majibu yako yapo hapo pembeni yako. Baada ya kuwapa maji na kunywa kilichofuata kilikuwa ni kukemewa, kwa nini awakemee? Kwa sababu walimuona Mungu tangu mwanzo lakini kwa nini walikuwa wanamtilia mashaka? Wangemwambia Musa tunakiu na si kuanza kunung’unika.

Likitokea jambo gumu katika maisha yako acha kunung’unika uliza kwa upole kwani majibu yake yapo. Hapa wamama mnapaswa kuponyeka, unapoona jambo haulielewi kwa mumeo uliza ujibiwe na si kuanza kunung’unika kwa maana mengine ni hisia zako, unahisi hakupendi lakini sio kweli, sasa badala ya kuanzisha ugomvi muulize kwa upole utajibiwa.

akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

Kutoka 15:26

Kama tutaisikia sauti ya Bwana hata kugombana hatutagombana kamwe. Mungu hapendi uone tatizo la Mwenzako, bali atapenda kwanza ujione matatizo yako. Hapa kuna mambo ya msingi matatu anayoyaelezea!

 • Magonjwa: ndiyo yanaangamiza zaidi ya kitu chochote.
 • Kuna mambo ambayo yanahusu mambo wasiomjua Mungu nakuna mambo ambayo yanahusu wanaojua Mungu. Hivyo kuna mambo ambayo halitakiwi yawasumbue watu wamjuao Mungu. Sasa inashangaza kuona watu wanaomjua Mungu wanasumbuliwa na mambo ambayo yanatakiwa kuwasubua wasiomjua Mungu.
 • Mungu anatuonesha kwamba yanayoendelea kwa wasiomjua Mungu na wamjuao Mungu ni yeye anayeyaruhusu. Tunajifunza kwamba Mungu yuko juu ya yote! Yaani alimpa Musa nguvu na Akampa Farao wimbo!

Mungu amesema hivi, kama utasikia yale yaliyokuwa yanakutesa yataondoka kwako.

MAOMBI:

 1. Ee Baba wa Mbinguni, naoba unipe neema ya kusikia na kuzingatia kile ninachosikia.
 2. Baba kwa Jina la Yesu Kristo naomba unifikishe salama mwisho wa safari hii. Nakupenda baba yangu!

MTUMISHI NI YUPI?

Uko njiani kuelekea mpenyo wa kiroho katika maisha yako ambao utakupeleka mbali sana zaidi ya matarajio yako uliyowahi kujiwekea. Nakuhakikishia kwamba kwa kadri utakavyozidi kusoma na kuongeza kweli hizi ndani ya roho yako, mstari kwa mstari na amri kwa amri, hutakuwa kama ulivyokuwa. Maisha yako yatabadilishwa, utapokea upako mpya wa nguvu za Mungu. Utajua namna ya kuzitenda kazi za Mungu!

Lengo kubwa la masomo haya ni kukufanya uweze kutoka katika hali ya mazoea na kuingia katika hatua ya viwango vipya, kuwa mpya kabisa na chombo chenye ufanisi mara mia. Yaani utakuwa ni mtumishi ambaye Mungu na watu wanajivunia uwepo wako maana utakuwa mwanajeshi ambaye unawafugua watu kutoka kwenye vifungo na utumwa wa adui katili, shetani. Na hii ndiyo kazi ya Mungu.

Katika mfululizo wa fundisho hili kwa yeyote atakaye zingatia sana jiandae kuingia kiwango kikubwa ambacho hujawahi kufikiria kufikia na hujawawahi kuwa nacho. Mungu tunayemtumikia ni Mungu ambaye hana mipaka, tunahitaji kufikia kiwango cha kuwa na nguvu za Mungu ambapo hatutazuiliwa na chochote.

UMEITWA ILI KUTUMIKA

Mikononi mwako kuna kazi za badaye za Mungu. Huduma ya kufanya kazi za Mungu si ya madhabahuni tu, maana wengi wanajiona hawahusiki tunapozungumzia huduma. Siku za leo, neno mtumishi tunalielewa kama ni la watu ambao wameenda shule za Biblia au seminari. Lakini tafsiri ya neno mtumishi kwa Kigriki ni kutumika. Yesu alilisitiza sana umuhimu wa kuwa watumishi. Tunaliona hili katika aya ifuatayo ambapo maneno yote mawili yametumika:

📖 “Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; 27 na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; 28 kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi”.

Mathayo 20:26-28

Maana halisi ya neno “mtumishi” linakuja kupatikana hapa. Yesu alisisitiza sana umuhimu uvumilivu wa kweli kwa mtu ambaye kweli anataka kutumika. Kwa maneno mengine niseme kwamba, kabla hujawa mtumishi lazima uwe tayari kujitoa (kwa kutoa muda wako, kipaji chako, fedha zako na chochote ulichonacho)kama Yesu alivyojitoa kama fidia ya wengi.

Sisi sote, uwe daktari, mwanasheria, mhasibu, mke wa nyumbani, mjane na kila mtu anayesema Yesu ni Bwana anaweza kuwa mtumishi kwenye maana ya neno na “kuzitenda kazi za Mungu”.

Wazo kuu

Ni kwamba kila mshirika wa kanisa la kwanza alikuwa mtumishi. Mtume Paulo alimuagiza Timotheo kuwashirikisha wengine kweli aliyoiona na kusikia.

📖 Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.

2 Timotheo 2:2

Inaonesha kuwa kila mtu katika kanisa la Kwanza alikuwa mtumishi japo sio wote walihubiri kama Petro na Paulo ingawa walikuwa ni watumishi. Neno la Mungu likaenea nyumba kwa nyumba. Hatuwezi kuufikia ulimwengu wote kwa kile kiitwacho eti utumishi wa madhabahuni tu, kila mshirika wa Mwili wa Kristo ni Mtumishi. Ni kweli huduma tano zilikuwepo katika kanisa la kwanza, lakini zilitenda kazi sawa na mpango wa Mungu. Kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwakamilisha watakatifu ili waweze kutenda kazi ya huduma! Na kila mtu akawamtumishi.

Wanawake waliosafiri pamoja na Bwana Yesu na wanafunzi walifanya kazi ya kupika chakula, lakini pia ndiyo walikuwa wa kwanza kubeba habari za kufufuka kwa Bwana Yesu kuwapelekea wanafunzi. Dorkasi alitumika kupanda mbegu na kugawa nguo kwa wahitaji. Stephano alikuwa mmoja wa watu saba waliochaguliwa kwenda kulikuza kanisa na akadhihirisha ishara na miujiza kwa watu wake.

📖 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

Waefeso 4:11-12 “

Mungu anataka akutumie kwa namna yako

Mungu anataka uwe mwakililishi wake, ukitoa uthibitisho wa kwamba Yesu yu hai. Giza la dhambi limetawala mazingira yakuzungukayo na anataka wewe uweze kuangaza kama nuru. Ametoa nafasi ambayo wewe pekee unaweza kuijaza. Wenye dhambi wanatakiwa waone wewe unavyowamulikia na wakufuate toka mbali. Mungu hataki watakatifu waondoke duniani (Zaburi 16:3). Anataka watumishi wote kwa kazi zao waweze kuangaza nuru wanapofanyia kazi.

📖 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. 15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. 16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Mathayo 5:14:-16

Mimi na wewe tunao wajibu wa aina moja, na kwa wajibu huu Bwana Yesu ametupatia nguvu na uwezo ambao unatufanya tuwe washindi na kuangaza kama nuru katika dunia hii, tukiwaleta waume kwa wake kwa Kristo. Mimi na wewe tu watumishi tunaotakwa kufanya kazi kuu mbili. (Somo litaendelea kesho)

🗣 TUOMBE

 1. Asante Baba Mungu kwa chakula hiki cha kiroho kilichonifikia.
 2. kwa jina la Yesu, ninaomba achilia upako wako – ili kila asomaye ujumbe huu ajitiishe kwako tangu sasa. Mpe ufahamu kwamba chapisho hili haliko mikoni mwake kwa bahati mbaya, bali ni kwa kusudi lako, hivyo ninaomba umtumie kwa utukufu na heshima yako.

Unaweza kujiunga kwenye group la PASTORBON kwa kujaza fomu hapa chini: http://forms.gle/957djapjw8gFLkF36

YUKO MLANGONI

Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami

Ufunuo wa Yohana 3:20

Soma;

Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. 20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. 21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.

Ufunuo wa Yohana 3:19-22

Mungu ni wa Utaratibu, na Mbinguni ni mahali ambapo utaratibu upo. Kuna Itifaki ya hali ya juu sana mbinguni na mamlaka ambayo lazima iheshimike. Hivyo tunapo msogelea Mungu kuna namna ya kumwendea. Namna ya kuingia ndani ya nyumba au chumba inategemea kwamba utakaribishwa au utafukuzwa. Unatambua kuwa hata Mungu mwenyewe anajibana na kanuni ya utaratibu. Yesu alisema;

“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.”

Ufunuo wa Yohana 3:20

Ingawa Mungu alituumba, bado inamlazimu abishe hodi na anasubiri akaribishwe kabla hajaingia moyoni mwetu. Hata kama aliweka nafasi ndani ya moyo wako kwa ajili yake mwenyewe, na bado hatumii nguvu kuingia ndani ya moyo wetu. Ni jukumu lako kuamua kama aingie au asiingie kwako.

Ktika Mwanzo 18:1-8, tunaona Ibrahim aliona Wageni kutoka mbinguni karibu na hema lake. Alipowaona akawakimbilia, akawalaki na kuwandalia chakula waburudike. Alionesha wema wa hali ya juu sana kwao. Ukilitazama hili tukio utaona kuwa Mungu alisimama pembeni akisubiri wamkaribishe. Vilevile, katika Mwanzo 19:1-3 tunaona Lutu anawakaribisha malaika wawili katika Sodoma akawasihi sana waingie nyumbani kwake waweze kulala na kuoga.

Pia 2 Wafalme 4:8 Elisha alikuwa anapata njiani mwanamke mmoja wa Shunemu alimkaibisha nyumbani kwa chakula na alikuwa hata hana njaa, lakini yule mwanamke alimng’ang’ania aingie ndani. Baada ya hapo, ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.

 1. Mungu anasubiri umkaribishe kwa sababu ya unyenyekevu wake. Na ni kwa sababu hataki kulazimisha kuingia ndani yetu.
 2. Alituumba sisi na uhuru wa kimaadili kama mawakili na si maroboti au mizimu.
 3. Anataka tuwe huwe huru kuonesha mapenzi yetu.
 4. Anataka tuwe huru kubeba mizigo ya matendo yetu ili tusije tukamtwisha lawama kwa matendo yetu wetu.
 5. Anataka kupima kama kweli tunampenda au la.

Kama bado hujaokoka, tambua kuwa unamtesa Mwokozi siku ulizoishi. Tafadhari itikia hodi yake kwenye mlango wa moyo wako. Tafadhari mkaribishe Yesu ndani, na ujisalimishe mzima mzima kwake. Kufanya hivi si amri ni maamuzi yako.

Chukua Hatua: Mkaribishe Yesu kwenye kila eneo la maisha yako ambayo ulimfungia nje.

Mtoto Lazima Akue

Mathayo 28:18-20.

Hapo Tunajifunza juu ya AGIZO KUU LA YESU KWA KANISA.

Kwenda, Kusababisha, kuwabatiza, kuwafundisha ndipo ile mamlaka wataiona ikitenda kazi siku zote pamoja nao. Yesu yupo hayo yakitimizwa nasi. Ndipo tutafurahia wokovu wetu hapa duniani.

2 Petro 3:18 “Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.”

Mpango wa Mungu ni kwamba watoto wakue na kuwa wana. Kwa namna gani mtoto wa kiroho anaweza kukua na kuwa mwana?

1 Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”

Hili ni eneo ambalo linaleta changamoto sana katika kanisa la leo maana wengi wanakataa mafundisho wa kukulia wokovu. Ama wazazi wa kiroho wamejua kuzaa tu lakini watoto wana njaa kali na kuugua kwashakoo. Mtume Petro anaweka wazi Ukweli kwa mtu asiyejifunza na kukomaa kiroho ni kazi sana kumshinda shetani. Cha kushangaza akawa amezungumzia nyaraka za Paulo ambazo ni ngumu kueleweka kwa mtu asiyekaa darasani na kujifunza. Hivyo wengi wasioelewa nyaraka za Paulo wakajituka wanasoma na kuyachukulia mambo kijuu juu sana na kutohoa andiko kama lilivyo.

Matendo 2:41-43 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. 42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume.”

Waabuduo Katika Roho Na Kweli

Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

https://www.facebook.com/efathambinga
Wana wa Mungu wakimfanyia Mungu wao Ibada.

Si matendo yote ya ibada ambayo Mungu anayakubali, kwa sababu si wote wamwabuduo ni waabudu halisi. Ukweli huu ulifunuliwa na Yesu alipokuwa anafanya mazungumzo na mama Msamaria katika kisima cha Yakobo. Alifunua pia ukweli mkubwa juu ya ibada ambayo tunatakiwa kuzingatia sana endapo tunataka ibada yetu ikubalike na Mungu.

Jambo la kwanza kuelewa ni kwamba kila “Mungu” ambaye anapatikana eneo fulani tu si Mungu wa kweli na hatakiwi kuabudiwa. Ibada inayofanyika kwa Mungu wa namna hii ni ibada feki. Ibada ya Mungu wa kweli haihusiani na kwenda njiapanda ambapo barabara tatu zinakutana kuweka chakula ili Mungu aje ale. Mtume Paulo alikutana na waabuduo namna hii katika milima ya Mars huko Athene (Matendo ya Mitume 17:22-31). Mungu wa Kweli anaelezewa na Mtunzi wa Zaburi katika Zaburi 8:1

Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;”

Ukweli mwingine ambao Bwana Yesu alitufunulia ni kwamba mungu yeyote ambao hana mahusiano ya ubaba na waabuduo huyu hastahili kuabudiwa nasi. Mtu yeyote anayemwabudu Mungu kwa namna hii si mwabudu halisi. Ndiyo maana Yesu alikuja kutufanya sisi wa Baba Yake. Na hata alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake namna ya kuomba, alimwelezea Mungu wa kweli kama “Baba” (Luka 11:2). Zaidi sana, Bwana Yesu alitufunulia kuwa ibada yetu kwa Mungu si halisi kama hatumjui Mungu tunaye mwabudu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo kuwatambulisha watu wa Athene kuwa walikuwa wanaabudu kwa ujinga (Matendo ya Mitume 17:23). Alijaribu kuwafundisha kwamba ni kosa kumwakilisha kichwa cha Mungu na dhahabu, fedha, au jiwe lililo chorwa kisanaa na vitu vya kibinadamu (Matendo ya Mitume 17:29). Hakuna mwabudu ambaye kwa ujinga akafikiri kuwa Mungu Mtakatifu atakubali ibada toka kwa mtu ambaye maisha yake yametawaliwa na dhambi za uongo, kujifanya na kila aina ya maadili mabaya na uovu.

Ibada ya kweli inahusiana na kumwabudu Mungu wa kweli katika roho na kweli. Lazima tumwabuduo Mungu katika roho kwa sababu Mungu ni Roho, na ni kwa roho pekee tunaweza tukaendana na Roho Yake. Kumwabudu Mungu katika roho ina maana kufanya kile anachokuagiza ufanye katika akili ya kiroho ya imani. Kuna mambo ambayo Roho Mtakatifu wa Mungu angetaka sisi tufanye lakini tungeliona kwa macho yetu ya kimwili, ni magumu kuyaelewa. Kwa mfano, pale Mungu alipo muagiza Nuhu kujenga safina kubwa sana katika nchi kavu, kwa watu wa kizazi chake, hili halikuwa jambo lenye maana la kulifanya. Kwamba mtu lazima awe na mme au mke mmoja “haijarishi pana ubaya au wema” watu hawaoni umuhimu lakini ndivyo Mungu wetu atakavyo katika Neno lake. Mwabudu halisi hataweza kusema uongo hata kama kuna madhara yanayoweza kumpata kupitia Ukweli wake. Kwa mwabudu halisi kuwa mkweli si kwa ajili ya mtu bali kwa Mungu ajuaye yote.

Yohana 4:21-24 “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Ombi la Msingi: Baba neema ya kuishi maisha yanayokunalika kukuabudu wewe kupitia Roho Mtakatifu wako, katika Jina la Yesu.