KWA NINI WAKRISTO WENGI HAWAONI NGUVU ZA MUNGU?

Wakristo wengi wanaufahamu msalaba wa YESU, unaowapa msamaha wa dhambi. Lakini wengi hawajawahi kuchukua hatua ya UFUFUO wa Yesu Kristo. Maana Msalaba ni Upendo wa Mungu na Ufufuo ni nguvu ya Mungu.

Tunapochukua hatua ya kuhamia katika msamaha wa dhambi na nguvu ya ufufuo wa Yesu Kristo. Ndipo anapodhirisha ushindi wake katika maisha yetu na ya wengine’.

Tunahitaji vyote (upendo na nguvu). Bila Upendo Nguvu zake zitatuharibu au tutaharibu wengine. Na bila ya nguvu Upendo wake hauna kazi. Wakristo wengi wana upendo kwa Mungu lakini hawana nguvu ya kushinda magonjwa, nguvu za giza, uovu, na nguvu za kipepo – hujitukuta wakishindwa vita.

BAADHI YA CHANGAMOTO ZA MTUMISHI

Mtumishi wa Mungu lazima awe makini sana na baadhi ya vitu, ili mwishowe asije akaangukia mikononi mwa ibilisi. Changamoto kubwa ni hizi zifuatazo: – 

 1. Nguvu
 • Nguvu inaweza kuua

Nguvu inasidia sana kwenye ulinzi. Tunaona 2 Wafalme 1:9-12, ambapo tunaona maaskari waligeuzwa majivu palepale. Hii ndiyo nguvu. Mungu wa Eliya ndiye Mungu wako, ile nguvu bado ipo hata sasa kama ilivyokuwa wakati ule wa Elia. Ukiwa na nguvu ya Mungu unaweza kumshughulikia adui. Nguvu ni nzuri lakini lazima idhibitiwe.

Kama Mungu ataweka nguvu kubwa kwa mtu ambaye hawezi kuitawala, kutatokea uharibifu mwingi sana. Mungu hawezi kuachilia nguvu zake kwa mtu ambaye hawezi kuitumia vizuri. Hebu fikiri mtu kichaa akipewa bomu nini kitatokea? Kama bado una hasira sahau kupata nguvu ya Mungu.

 • Nguvu inaweza kukuharibu

2 Samweli 11:1-27, hapo tunaona nguvu ikimharibu Mfalme Daudi, alipopata cheo akiwa matembezini akaona mke wa mtu akioga, kama mfalme akatoa amri kuwa yule mwanamke apelekwe kwake. Yule mwanamke akapata ujauzito wake na alitumia nguvu zake kupanga mauaji ya mme wa yule mwanamke.

 • Nguvu inaweza kumwangamiza aliye ibeba.

Kwa kuwa nguvu za Mungu zinaweza kupelekea mtu kiburi. Katika Waamuzi 16, tunaona habari za Samsoni. Wazazi wake walimuonya asioe mwanamke ambaye hajaokoka, lakini hakuwasikiliza. Samsoni akaishia kuangamia.

 • Nguvu inaweza kuwa chanzo kikubwa cha majaribu.

Ukisoma Mathayo 3:16-17 na ukilinganisha na Mathayo 4:1-11, utagundua kuwa ghafla Yesu alipobatizwa ubatizo na Roho Mtakatifu ndipo ibilisi akampeleka katika majaribu mazito. Ibilisi alimuomba Yesu kutumia nguvu zake kubadili jiwe liwe mkate. Ibilisi alitaka Yesu atumie zile nguvu kujishibisha. Tambua kuwa ibilisi anaweza kukushawishi utumie nguvu ulizo nazo kujilimbikizia mali. Mungu akikupa kanisa la kuchunga usiligeuze kuwa chanzo chako cha kujipatia chakula. Haimaanishi kuwa ni kosa kanisa kukupa chakula bali nina maanisha wewe zingatia kufanya ya Bwana na Bwana atafanya yanayokuhusu.

 1. Kukosa uzoefu

Uzoefu ni mwalimu bora sana. Kuna faida kubwa sana za kujifunza kutokana na uzoefu wa watumishi waliotutangulia ili ujue namna gani ya kushinda. Maana uzoefu unaweza kujifunza kwa kutazama wengine au kwa kupitia mwenyewe.

Samweli alijifunza kwa Eli. Alitambua kwamba ni kwa sababu watoto wa Eli walikuwa wakicheza na sadaka za Mungu, walikosa nidhamu na kufanya uzinzi na kuchafua nyumba ya Mungu, ilipelekea Mungu kusema katika 1 Samweli 2:30:

Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.”

Samweli akalipata hili somo. Maisha yake yote na watoto wake walijizuia kabisa kuichafua madhabahu ya Mungu (1 Samweli 12:1-5).

Daudi alipata uzoefu kwa mfalme Sauli. Ndiyo maana katika 2 Samweli 6:14-22, alicheza mbele za Bwana kwa uwezo wake wote.

Mfalme Nebukadreza alijifunza kutokana na aliyoyapitia mwenyewe katika Danieli 4, Mungu alimuonya kupitia ndoto. Mungu akamwandalia na mpango wa kutafsiriwa ndoto, lakini akapuuzia onyo. Kwa miaka saba alikula majani kama mnyama ndipo akapata ufahamu na kutambua kuwa mfalme wa kweli ni Mungu.

Kama kuna somo moja kubwa la kujifunza kwa Farao, ni kwamba haiwezekani kupigana na Mungu na ukashinda. Maana Biblia inasema:

“Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.”

Warumi 9:17
 1. Uwezo wako.

Changamoto kubwa hapa ni kwamba Mungu ana vitu vingi sana na hata anapotupa anatoa kwa kadri ya wingi wa utajiri wake, lakini tatizo kubwa ni uwezo wa Mtumishi kuchukua kutoka kwa Mungu.

Zaburi 23:5 inasema:

Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika

Wakati wote Mungu anapotoa, anatoa mpaka mpokeaji anachanganyikiwa (Malaki 3:10, Mithali 3:9-10). Katika Yohana 2:1-11, katika harusi ya Kana, kilichotakiwa ilikuwa ni divai ili sherehe iishe salama. Lakini alitoa zaidi ya walichohitaji na ilikuwa divai bora sana. Mungu anasema endapo utayatenda mapenzi yake atakubariki kiasi kwamba baraka zitakuwa zikikukimbiza na kukupata.

Kama Mungu anajitosheleza kwa nini Mtumishi unakosa upako wa kutosha? Kwa nini unapungukiwa fedha? Kwa nini uko upande wa moto na bado umeoza? Kwa nini uko kwenye ukingo wa mto na bado una kiu?

 • Inawezekana unatamani vitu visivyo, pengine unatamani utajiri. Mithali 23:5 “Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni.” Maana mara nyingi wanaotamani mali hunaswa katika mtego.
 • Pengine unaomba Mungu akupe kutambulika. Yeremia 45:5 inasema “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema Bwana; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.”
 • Pengine unatafuta mamlaka. Mamlaka au nguvu inaua. Katika 2 Mambo ya Nyakati 26 mfalme Uzia alimlingana Bwana na akawa tajiri sana. baadaye akamkosea Mungu na akaangamizwa. Vivyo hivyo kwa Samsoni katika Waamuzi 14:1-3, Samsoni alisisitiza kwamba ataoa mahali ambapo si sahihi, kwa kutumia nguvu zake licha ya maonyo ya wazazi wake.

Una kiu kiasi gani kwa ajili ya mambo ya Mungu? Katika Mathayo 5:6 Biblia inasema:

Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”

Mathayo 5:6

Sababu ya kwa nini huna kitu inawezekana wewe bado ni bahili. Maana mtu bahili atazidi kuusogelea uhitaji daima. Mithali 11:24-25, inathibitisha hili:

Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.”

Mithali 11:24-25

Unachotoa kinaamua upate nini. Luka 6:38 inasema;

Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa

Luka 6:38

Ukuu unategemea sana kiasi gani unatoa na si muhimu sana kwamba una nini. Katika 2 Wafalme 4:8-17, mwanamke Mshunami aliitwa ‘mkuu’ si kwa sababu ya utajiri wake, ila kwa sababu alikuwa mtoaji sana. umewahi kutoa bila kuombwa? Je umewahi kujitoa kuomba kwa ajili ya mkubwa wako bila yeye kukuagiza?

Mwamba wa upako ni huduma ya kujichotea tu. Mungu akiona kwamba una hiari ya kutoa muda wako na nguvu kwa ajili ya wengine, upako utakujilia. Je uko tayari kufa ili wengine waishi? Kama kweli basi tambua Mungu atakuagiza umpelekee vyombo vyako tu ili yeye aweze kuvijaza mpaka vifurike na upako. Kama unatamani kutumia, kubali kutumiwa, ataleta upako kwako.

 1. Kujiongoza.

Hali ya kujiongoza inaanza pale ambapo unaona kama unabanwa, unaanza kuona kama umekua na unazuiliwa kupaa kama utakavyo. Unapoanza kuona hali ya kutofurahia utumishi wa kuwa chini ya mtu unatakiwa kuwa makini sana, inawezekana unataka kuanza kujiongoza.

Mwana mpotevu alikuwa na wazo la kutaka uhuru ili ajiongoze mwenyewe na akaanza kudai urithi wake.

Ole wa watoto waasi; asema Bwana; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi; 2 waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri. 3 Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu.”

Isaya 30:1-3

Baada ya Mwana mpotevu kuupata uhuru alioutaka zikaanza starehe, akaanza kujifurahisha. Akaanza kuishi atakavyo, alienda kwenye starehe kila siku. Lakini ikumbukwe kuwa uhuru ukizidi unasababisha kupoteza na kuharibikiwa. Na ukisha poteza ulichokuwa unajivunia ndipo aibu inakufuata. Unajua kuwa tawi la mti likikatwa toka kwenye shina, kwa kitambo fulani bado linaendelea kuwa majani yenye rangi ya kijani. Hii ni kwa sababu kunakuwa bado kuna virutubisho vimetunzwa kwenye tawi. Lakini vile virutubisho vya chakula vikiisha kinachofuata ni majani kukauka.

Watumishi wengi sana wanaojitafutia uhuru kwa matakwa yao wamejikuta wakiishia katika aibu kubwa baada ya kushindwa katika utumishi wao.

 1. Roho za mazoea.

Roho za mazoea zipo kwenye jamii nyingi na ni rahisi kuua kazi ya Mtumishi. Zinatokana na mwingiliano kati ya mtumishi na anaowaongoza, hali inayowapa nafasi ya kufahamu mambo mengi kuhusu Mtumishi wao. Anavyoweka watu karibu naye wanaingiwa na roho ya mazoea. Hata Bwana Yesu alipokutana na watu wa namna hii, aliwaombea na kuponya wachache tu kutokana na kuwa watu wa dharau.

Yesu Akasema, Amini, nawaambia ya kwamba, hakuna Nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.

Luka 4:24, 28-29

Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika Sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini.”

NGUVU

Mtume Paulo alipotoka jangwani baada ya Mungu kumchukua na kumbadilisha akiwa njiani kuelekea Dameski, aliweza kusema, “… mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu (Wagalatia 1:16)”

Alienda katika miji na kusema “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu”

“nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi. Nilikuwa mwanafunzi wa wanafunzi, nimekuwa Mwalimu wa Walimu. Mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo.”

“Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.”

Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. 5 Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, 6 kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”

Wafilipi 3:4-6.

MAFANIKIO MAPYA YA KIROHO

Lakini mtume Paulo anasema chochote

“Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo.”

Wafilipi 3:7-8

Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu”

1 Wakorintho 2:4

UDHIHIRISHO WA NGUVU

Paulo na washirika wengine wa kanisa la Mungu walisitaajabisha ulimwengu wa kisiasa wa kipindi walichoishi kwa nguvu ya Roho wa Mungu Anayeishi.

Kanisa la Yesu Kristo, lilizaliwa kupitia udhihirisho wa NGUVU ya kitume.

Je, leo tuna nini?

Tuna nadharia nyingi mno.

Tuna theolojia nyingi mno.

Tuna mafundisho mengi mno.

Lakina hatuna udhihirisho wa nguvu za Mungu!

Yesu Kristo anakuja mara ya pili na kanisa litanyakuliwa.

Je, umewahi kufikiri hata kwa dakika moja kwamba kanisa litanyakuliwa likiwa halina nguvu, lina anemia, limedhoofu, limelala, lisilojali hali iliyopo leo?

Kanisa lilinyakuliwa ni Bibi Harusi wa Kristo. Ni zawadi ya pekee atoayo Baba kwa mwanaye wa pekee, Yesu, kwa kazi yake ya Ukombozi aliyoikamilisha hapa dunia, kwa kuacha utukufu mkubwa uliomzunguka kule mbinguni na akachukua ufanano wa mwili wa dhambi, kwa kuvumilia mateso, kukataliwa na maumivu ili tu kwamba ajitoe kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima

Je, unafikiri kuwa Mungu ataridhika kuona alitoa zawadi ya pekee ya Mwanaye Yesu Kristo na kupitia maumivu makubwa kiasi kile na aone Bwana Harusi, anamletea kanisa nyonge kama tulionavyo leo?

Ukweli haiwezekani, lazima jambo fulani lotokee. Lazima tulifanye litokee. Nakutabilia kuwa moja ya mafanikio makubwa ambayo utayapata katika ulimwengu wa roho kwa jinsi ujio wa mara ya pili wa Yesu Kristo unakaribia ni:

Kanisa La Yesu Kristo Litanyakuliwa Likiwa Na Udhihirisho Wa Nguvu Za Mungu Za Ajabu Mno  Na  Roho Mtakatifu Atamwangwa Kuliko Hata Kanisa Lilivyokuwa Linaanza.

Kanisa lilizaliwa katika nguvu. Ilieleweka kabisa kuwa kanisa lina nguvu. Kulikuwa na miale ya moto. Kulikuwa na kunena kwa lugha mpya. Kulikuwa na nguvu. Unaweza kusoma kipande kidogo tu cha Matendo ya Mitume Kuhusu kanisa la kwanza na ukaona jinsi ambavyo hawa watu walitembea katika nguvu za Mungu. Kubwa tena kubwa mno. Watu walijaa nguvu.

Mungu alichukua wanaume na na wanawake wabishi, waoga, wasio na elimu, wasiojulikana, na wengine hata hawakujua hazina za dunia hii, lakini Mungu aliwasha moto wa nguvu za mbinguni ndani yao na wakaweza kuifagilia dunia kwa Yesu.

Hili linafananaje na kile ambacho tunakiona siku za leo?

Ninao ujasiri wa kukuambia kuwa mpaka leo bado sura ya mwisho ya kitabu cha matendo ya  Mitume wa dunia hii bado haijaandikwa na haijafungwa!

Siku moja nilipomaliza tu kuomba usiku wa saa nane, Bwana Yesu alikuja chumbani kwangu, mwili mzima ulizimia ganzi kwa kuona tu ule mwanga wake nakumbuka ilikuw ani Tarehe 27 Julai 2014. Bwana aliponitokea nguvu zote zikaisha na alikuja kuniambia tunifundishe viongozi, sikulala mpaka asubuhina kesho yake sikuweza kuhubiri nilisimulia tukio na kulia tuna watu walifunguliwa sana.

Kazi ya Mungu si kazi ya mtu, hivyo tunahitaji kuwa na vitendea kazi vya mwenye kazi, ambavyo ni Roho Mtakatifu na nguvu za Mungu.

Kwa kadri tunavyozidi kutamani kuwa karibu naye, nguvu, uwepo wake, upako, utukufu ufufuo wa Yesu Kristo na udhihirisho wa Roho Mtakatifu utakuja kwetu katika ulimwengu wa roho na kudhihirka katika ulimwengu wa kawaida (asili). Ukweli tunaenda katika viwango aambavyo macho hayajapata kuona wala masikio hayajawahikusikia, kabla ya unyakuo tutatembea katika viwango vikubwa na vya kushangaza mno.

Dunia nzima itajua kwamba Yesu yu Hai, kwamba ni Mwana wa Mungu,na kwamba alikuja huku duniani kwa kusudi. Wataona nguvu zake zikidhihirika ndaniya watu Wake kwa namna ya ajabu sana.

Yesu alisema;

Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”

Mathayo 24:14.

Tupo katika kipindi cha mpenyo (kufanikiwa), kipindi cha kutoa uthibitisho (ushuhuda) kwanguvu.

Tunaweza, ni lazima, tutafanya, acha kujiwazia huwezi, si wewe bali Mungu ndani yako. Vuka mipaka ya uwezo wako wa kufikiria.

🗣 OMBA:

 1. Omba Mungu mwenye nguvu, uliye Baba yangu nijalie Mtumishi wako, kufikia hatua yakudhihirisha nguvu zako, nina kiu na uwepo wako maishani mwangu, katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

Unaweza kujiunga kwenye group la Goodvine Discipleship School la WHATSAPP kwa kujaza fomu hapa chini:

http://forms.gle/957djapjw8gFLkF36

MAFANIKIO MAPYA YA KIROHO

Mungu ametupa maneno ya msingi yaliyo mazuri sana, ukweli mkubwa, ambao kiukweli unasaidia sana uwezo wetu wa kuelelewa mambo ya kiroho.

Ni hivi:

Mtu anaishi katika ulimwengu wa aina mbili. Anaishi katika ulimwengu wa asili na pia anaishi katika ulimwengu wa roho. Mambo yanayotokea katika ulimwengu huu wa asili yanaenda sambamba na matukio sawasawa katika ulimwengu wa roho.

MAMBO HAYA NI KWELI ILIYO SAMBAMBA

Tunaona matukio mengi yanayotokea duniani siku za leo. Kuna kitu kinatokea kwa mtu wa ulimwengu wa asili hii. Akili ya mtu, yaani uwezo wake wa kawaida ya ulimwengu huu wa asili unaongezeka sana. Siku hizi mwanadamu anaweza kufanya vitu ambavyo ukweli vilikuwa havifikiriki kufanyika na mtu yeyote miaka michache iliyopita. Vitu ambavyo vilichukuliwa kama ndoto tu au hadithi za kisayansi leo vimetimiana kuzidi kiwango cha hadithi za jana.

Neno la Mungu lilishatutabilia kuwa tunapokaribia siku za mwisho, uwezo wa mwanadamu, uwezo wake wa kiakili, utazidi kuimarika zaidi.

“… na maarifa yataongezeka.”

Danieli 12:4

Na hili linatokea kwa kiasi kikubwa hasa wakati huu ambao tunakaribia ujio wa pili wa Yesu Kristo. Ujio wa pili wa Yesu Kristo upo karibu sana. Ndiyo maana akili ya mtu wa asili ya ulimwengu huu inazidi kuwa kubwa zaidi katika nyakati zetu.

Mtu anafanya kitu ambacho katika ulimwengu huu ninakiita “Mafanikio.” Anafakiwa sana katika uwanja wa sayansi. Mafanikio katika madawa. Mafanikio katika teknolojia. Na mafanikio katika kila jitihada za kibinadamu.

Natabiri kuwa ujio wa Yesu hauko mbali sana toka sasa, na uwezo wa mwanadamu utaongezeka kila mara zaidi na zaidi mpaka Yesu anapokuja tena.

Sasa, swali ni hili, kama katika ulimwengu wa asili mafanikio ni makubwa kiasi hiki, nini kitatokea katika ulimwengu wa roho? Je, Mungu ataruhusu Mwili  wake, Kanisa Lake, kuwa katika kiwango cha chini cha maendeleo na mafanikio wakati dunia inainua viwango vyake vya maendeleo, maarifa na uwezo?

Hapana kabisa!

Kwa kadri kurudi kwa Yesu kunavyo karibia, kanisa la Yesu Kristo litazidi Kuinua viwango vya mafanikio ya kiroho zaidi ya ufahamu wa akili za mtu wa asili ya ulimwengu huu. Tutapata mafanikio bora sana ya kiroho ambayo yataenda sambamba na kinachoendelea duniani.

boniface evarist mwakisalu

Haya mafanikio yatakuja kwa njia nyingi.

Moja: Kanisa hili halikuzaliwa nyonge; halikuzaliwa na anemia; halikuzaliwa bila roho.

Wengine wanadhani kuwa kila anayoweza kuyafanya Mungu tayari yamekwisha kuonekana kwa wanadamu tayari. Hili si kweli. Kuna mambo ambayo bado hayajaingia hata kwenye moyo wa mwanadamu, wala macho bado hayajaona mambo ambayo Mungu amemuandalia mwanadamu.

“lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.”

1 Wakorintho 2:9

Tunapoteza mbio. Wasioamini uwepo wa Mungu wanapita Wakristo.

Uamsho wa maswala ya uchawi unafika mahali katika hatua ambayo hata kuna mashule yanafundisha rasmi, kwa kusoma kisoma vitabu au Kutazama filamu za akina mfano  za akina Harry Potters zinafundishwa na mashule mengi hayaweki kipaumbele kwenye kufundisha Biblia.

Tukitazama nyuma miaka 2000 iliyopita ya kanisa la kwanza, tunakuta kwamba miaka 200 baada ya Yesu kufa pale msalabani, wanafunzi Wake kwa nia na kusudi moja waliweza kuhubiri injili duniani. Kwa ujumla dunia nzima ilikuwa katika ushawishi wa ukristo kwa namna fulani.

Nini kilitokea?

Kwa jinsi tunavyozidi kuifuatilia historia ya kanisa, tunagundua kuwa kipindi cha Enzi za Giza kilileta muundo wa kidini. Ukristo ulianza kulegezwa mpaka ikifika wakati ukawa kama umepotea. Udhihirisho wa nguvu za Mungu ukaanza kupungua hasa walipoanza kuweka utaratibu wa mahubiri ya pointi tatu kwa ibada. Ingawa, kanisa halikuanza kwa namna hii.

SI KWA WAHUBIRI WA KUPATA FEDHA

Miaka 2000 iliyopita kanisa halikuzaliwa kwa mtu ambaye atahubiri ili apate fedha. Halikuzaliwa kupitia ujanja wa mahubiri ambao tunauona katika Injili ya siku hizi. Ni rahisi sana kuhubiri siku hizi kwa sababu hatuhangahiki tena kuthibitisha chochote kama ilivyokuwa zamani.

Ili uweze kuhubiri siku hizi inakupasa tu uwe msomi wa chuo kikuu au seminari au mtu yeyote anayejua kuongea vizuri na kuchekesha. Unaweza tu kuzipangilia pointi zako tatu, utaelezea ya kwanza, ya pili na ya tatu kisha hitimisho. Unaingizia stori nzuri na ucheshi kidogo ambao umeutengeneza. Ukiweza tu kuongelea nguvu ya kuwaza chanya na nguvu ya akili juu ya jambo fulani, hapo unakuwa tayari umefanikiwa.

Namshukuru Mungu kwa wahubiri wakubwa. Tunawahubiri wakubwa sana ambao dunia haijawahi kuwa nao, lakini walimwengu wanaohubiriwa wanaenda kuzimu. Unakuta duniani hapa, ikiwemo Tanzania na nchi kubwa kama Marekani, Uingereza, Afrika ya Kusini utakuta redio nyingi na mitandao ya kijamii na vipindi vya TV, vina mahubiri ya kuwafikia watu. Bado hawajaweza kuzuia ushawishi wa maswala ya ngono, ndoa za jinsia moja, ulevi, matumizi ya madawa na maovu mengine. Hatujaweza kuzuia.

Kanisa la mwanzo halikuzaliwa kwa kuwa Mhubiri sana, wala halikuzaliwa kwa kuwadanganya watu.

Kanisa lilizaliwa kwa udhihirisho wa nguvu.

Yesu alisema:

Mtapokea NGUVU.

Matendo ya Mitume 1:8

Baada ya wanafunzi kumwagiwa Roho Mtakatifu, walikuwa wakishangilia kwa ushawishi wa nguvu.

Kuna watu walisema, “wamelewa kwa mvinyo mpya.

Lakini Petro akasema, “Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa

Alisema:

“lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, 17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto”.

Matendo ya Mitume 2:16-17.

Fuatilia kesho muendelezo wa somo la NGUVU….

🗣 OMBA:

 1. Omba Mungu, akupe neema ya kubeba injili yako sawa na mapenzi yako na si kwa jinsi ya kibinadamu, katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

Unaweza kujiunga kwenye group la Goodvine Discipleship School la WHATSAPP kwa kubonyeza picha hapa chini:

Ili uweze kupata mafunzo ya kila siku ungana na GOODVINE WhatsApp.

Mafundisho

usomaji wa Biblia

Ukiri wa kila siku

Maombi

cheti cha baada ya kumaliza kozi

na mengineyo mengi.

MUNGU ANATAKA WEWE UTOE UTHIBITISHO, POPOTE ULIPO, POPOTE UENDAPO

Mfulilizo wa masomo haya utakufanya uzipokee funguo zote zitakazokufanya wewe uwe mtumishi bora na uweze kuwatumikia waliopotea na ulimwengu unaoangamia. Utafahamu namna ya kutenda katika uweza wa Roho Mtakatifu. Inawezekana sio mtume, nabii, mchungaji, mwalimu au mwinjilisti, lakini nikwambie hivi, “utaweza kutoa uthibitisho”

 • Usiogope na usiwe na aibu.
 • Nenda kwa Jina la Yesu.
 • Ruhusu nguvu ya Mungu ijae ndani yako.
 • Kwa pamoja tutaweza kusonga mbele, na umtukuze Mungu maana tu washindi.

Tazama viganja vya mikono yako na msikilize Roho Mtakatifu anachoongea na wewe. Ubadaye wa ufalme wa Mungu upo mikononi mwao watafutao jibu la swali hili:

📖 Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?

Yohana 6:28

Kabla sijakupeleka hatua nyingine ya fundisho hili, tambua kuwa nakuombea sana ujue cha kufanya ili uweze kutokeza kama ushuhuda unaoishi siku zijazo.

Kwa neema na kibali cha Mungu kupitia ukombozi sisi ni watu wa daraja la juu na wa kufanya vitu vikubwa mno lakini lazima tuwajibike ili kufikia ukuu. Namsihi Mungu akupe neema na kibali cha kufikia ndoto yako. Amina!

MEI 2020 ZINGATIA HAYA:

Je, Roho Mtakatifu anasemaje kwa ajili ya huu mwezi wa Mei 2020?

 • Mungu atasamehe watu wengi mno nao wataingia kwenye maongozi ya kiungu katika safari yetu ya maisha (Zaburi 23:1-6, Isaya 48:21).
 • Kwa kufuata maongozi ya Kiungu, ndipo tunafikia kwenye daraja la kufika kwenye nchi ya ahadi   (Hesabu 9:15-23, Kutoka 13:17-18)
 • Maongozi ya kiungu inawezekana ‘yasiwe na maana’ kwa matakwa ya wanadamu, ila ndiyo njia pekee ya kupitia ili ufanikiwe (Isaya 55:8, 2 Wakorintho 11:3).
 • Kwa kuwa Mungu anaijua kesho, kama anavyiojua leo, pia anajua mwisho toka mwanzo. Hivyo kumfuata yeye kutakuhakikishia kufika katika nchi ya ahadi (Isaya 46:9-10)
 • Kulingana na Neno la Mungu, maongozi ya kiungu ndilo geti la kuingia katika utendaji wa mambo makuu. Kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu na Isaka (Isaya 51:1-3, Mwanzo 12:1-3, Mwanzo 26:1, 12-14).
 • Pia lazima tuelewe kwamba hatuna mkato wa kufikia hatima zetu kama waamini, ila tu kutafika kwa kufuata hatua kwa hatua kama tunavyooongozwa na Roho wa Mungu (Kutoka 13:17-18, Kutoka 23:20, Kumbukumbu la Torati 7:22).
 • Maongozi ya kiroho yanatuhakikishia usalama na kufikia hatma yenye utukufu (Kutoka 23:30, Kumbukumbu la Torati 5:32-33).
 • Hakikisha unakuwa mtu wa rohoni ili uweze kupata maongozi ya Kiungu. (Wagalatia 5:25, Ufunuo 1:10, Isaya 30:20-21).
 • Ingawa, kufuata maongozi ya kiungu ni maamuzi yako, siyo lazima (Kumbukumbu la Torati 30:19, Luka 9:57-61)

Kama sote tujuavyo kuwa iko njia ionekanyo ni sahihi kwa mtu, ila mwisho wa njia zao ni mauti (Mithali 14:12, Mithali 16:25).

Watu wakuu na matajiri waliokuwepo mwanzo na wameandikwa kwenye Biblia ni watu walioongozwa kiungu. Mfano wao ni Ibrahimu, Isaka, Musa, Gidioni, Daudi na wengineo wengi. Hii ni zamu yako kuongozwa na Mungu.

Hivyo basi, mtazamo wa kinabii kwa mwezi Mei 2020 ni:

🗣 TANGAZA KUWA:

 1. BWANA, KATIKA JINA TAKATIFU LA YESU KRISTO, MIMI NI MWANAO, NIMESAMEHEWA DHAMBI NA DHAMBI SI SEHEMU YANGU TENA, MIMI NI NURU NA NITAWAMULIKIA WENGINE NURU YAKO.
 2. BWANA, NAKUBALI NA NIKO TAYARI KUONGOZWA NA WEWE TANGULIA MBELE YANGU, ONGOZA NJIA ZANGU.
 3. KUANZIA LEO, NIMECHAGUA KUFUATA MAONGOZI YA KIUNGU ILI UTHIBITISHE KESHO YANGU, KESHO YA BIASHARA YANGU, KESHO YA NDOA YANGU, KESHO YA UTUMISHI WANGU, KESHO YA KAZI YANGU N.K

Unaweza kujiunga kwenye group la PASTORBON WHATSAPP kwa kujaza fomu hapa chini: http://forms.gle/957djapjw8gFLkF36

WATOA UTHIBITISHO -II

TUFANYAJE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU?

📖 Yohana 6:28 Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?

Mungu anaendelea kuongea na watumishi wake kama alivyoongea na akina Ibrahimu, Henoko, Musa, Eliya, Isaya na wengineo wengi. Bado anaongea na watu wake kama zamani, na ujumbe huu ni maongezi yake kwetu. Katika sura ya 18 ya kitabu cha Mwanzo tunaona Mungu alipanga kuiangamiza Sodoma na Gomora kutokana na maovu yao, lakini ili atimize hilo, tunasoma swali la ufunuo:

📖 Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo? Mwanzo 18:17

Bwana alitaka kumshirikisha mtumishi wake. Bwana aliongea na mtumishi wake na akamwambia mipango yake. Na katika mstari wa 19 anafunua siri kwa nini aliamua kuongea na Ibrahimu. Alisema:

📖 Kwa maana nimemjua …

Mungu alimjua Ibrahimu kuwa atafanya kwa kipau mbele jambo ambalo Bwana atamwambia. Bwana alijua kuwa Ibarahimu atamwamini huyu mtu na ataweza kuongea naye kibinadamu. Yakobo anatuambia kwamba Ibrahimu aliitwa “rafiki wa Mungu” (Yakoo 2:23)

Musa pia alikuwa rafiki wa Mungu ambaye waliweza kuongea ana kwa ana na kumfunulia mipango yake:

📖 Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake … Kutoka 33:11

📖 Amosi 3:7 inasema “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”

Ahadi hizi siyo tu za kipindi cha zamani, maana Mungu tuliye naye ni Mungu ambaye kamwe habadiliki, yupo nyakati zote na habadiliki. Mungu hajaacha kuongea na watu wake katika mambo yake. Anataka kujifunua kwetu mara zote, lakini anajifunua kwa watu waaminifu kama alivyokuwa anajifunua kwao zamani.

Mwaka 2004 nilihudhuria mkutano wa kiroho katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, uliongozwa na Mwalimu Christopher Mwakasege, kwa mara ya kwanza nilisikia sauti ikiongea nami kama wazo kuwa “jiandae ukikua utafanya kazi hii, utaenda mataifa mengi kwa ajili yangu”. Haikupita nusu saa nikamsikia Mwalimu pale madhabahuni akisema kuna watoto wako hapa Bwana anataka niwaombee kwa kazi ya injili siku zijazo, tukapita mbele akaomba kuna maneno aliniambia nilimshangaa sana Mungu. Mwaka 2006 nilifunga siku tatu na kwa mara ya kwanza tulikuwa mlimani nikiomba na rafiki yangu Gasper Mungu akaongea nami tena, na hapo alinionyesha jinsi ambavyo atawaadhibu watendao dhambi – siwezi kusahau hadi leo. Toka kipindi hicho nilianza kujitambua kuwa mimi nitakuwa mtumishi wa Mungu!

Mwaka 2012 ndipo alipoongea nami tena waziwazi, nikiwa nasali kanisa langu lilelile la KKKT, akaniambia sasa nataka uanze kujifunza namna ya kunitumikia na nitakupeleka mahali pa kukua kiroho kwa haraka, nikapewa kuchagua mtumishi wa kunilea mmoja yuko Nigeria na mwingine yuko Tanzania. Katika ndoto hiyo niliambiwa changua nani akulee kati ya hao – sikujibu chochote, ndipo nikafunga na baada ya mfungo wa siku tatu nikajikuta jumapili ya disemba 16, 2012 nikiwa njiani kwenda kanisani (Lutheran), likaja wazo kwa nguvu sana kwamba tafuta kanisa la Efatha hapa Songea, sikujua kama pana kanisa la Efatha Songea, nilipowauliza watu wakaniambia lipo Mkuzo, hata mtaa wa Mkuzo pia sikuwahi kuusikia. Nikapanda daladala na nikafanikiwa kufika hapo na ndipo nikamkuta mmoja wa wale niliombiwa nichague anilee – Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira na akaongoza ibada na nikawa na amani tele ya kuokoka siku hiyo. Na kweli nikaokoka kwa kuongozwa na yeye mwenyewe, baada ya ibada akaniambia ukimaliza chuo kikuu unifuate Mwenge, na hata sasa ndiye aliyeniingiza rasmi kwenye utumishi huu wa kichungaji. Siku moja Bwana Yesu aliniambia usendelee kuhangaika kutafuta wa kumuoa bali mke ambaye utamuoa ni Vaileth, na siku nyingine akanitokea waziwazi na kusema fundisha viongozi wako (Julai 24, 2014). Sitaeleza yote hapa!

Wazo kuu

Mungu bado anaongea na watu wake hata leo, anasema kwa njia nyingi ikiwemo; Neno lake, muziki, watu, matukio yanayojirudia, mazingira, ndoto, maono, Roho Mtakatifu, mawazo, sauti ya wazi, amani na ishara namiujiza isiyo ya kawaida. Mungu daima anatuongoza, anatuelekeza, anatuonya, anatutia moyo, anatuahidi, anatufurahisha, tunatakiwa kuwa makini na kuuijua sauti yake ili tusiwe viziwi wa kiroho. Tutaweza kuzitenda kazi zake endapo tu tutafanya bidii kuisikia sauti yake hata kama dunia imejaa mashaka na mitazamo mingi.

Hatua za kusikia sauti ya Mungu

 1. Tuliza akili yako.
 2. Mfanye Mungu kuwa Mshauri wako namba moja.
 3. Uwe makini.
 4. Imarisha uhusiano wako na Mungu.
 5. Soma Biblia yako
 6. Fanya ibada (abudu)
 7. Daima tulia na kusikiliza

Je, unazifahamu njia nyingine ambazo Mungu anatumia kuongea na watu? Ziweke kwenye comment hapa chini.

🗣 TUOMBE

 1. Ee Baba, nisaidie kujua njia zako kwa namna nyepesi, niweze kukutumikia na kuuleta ulimwengu kwa Yesu Kristo!

Unaweza kujiunga kwenye group la PASTORBON la WhatsAPP kwa kujaza fomu hapa chini: https://forms.gle/957djapjw8gFLkF36

Pia, Like page ya Facebook: https://fb.me/boniemwa