SAFARI YA UKOMBOZI

👤 Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira [🇹🇿]

Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

Waefeso 4:12-14

Lengo kubwa la mafundisho haya ili tuweze kukamilishwa na kujengwa ili kufika pale Mungu alipotuandalia pasipo kupoteza mwelekeo wa udanganyifu wa ibilisi. Kuna vitu vitakuja kutoka kwa ibilisi na vitakusukuma huku na kule au kuna watu watakuja na ufahamu wao na kwa kupitia neno la Mungu na watakusukuma na wewe kwa sababu hukumbuki Neno linasema nini unajikuta umeingia mahali ambapo hukutakiwa uingie.

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 2 Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

Kutoka 15:1-2

Mungu anapokupa kitu ambacho hukustahili inabidi umsifu mfano kupata mke au mme ni mpango wa Mungu. Tambua kuwa hata kupata mtoto ni mkono wa Mungu – ina maana kuwa sio kwa nguvu zako bali kwa mkono wa Bwana.  Kuna mambo makuu mawili ambayo tunajifunza hapa:

 1. Kujua kipi katika maisha yako ni mkono wa Mungu na kipi ni nguvu ya Mungu.
 2. Baada ya kugundua peleka shukrani au sifa kama ni wimbo au kwa chochote. Kuna vitu vingine ambavyo ni kwa uwezo wako: mfano kuamka asubuhi sio nguvu zako. Wewe ukiamkaasbuhi sio uwezo wako, wengine akiamka asubuhi anakuwa amekufa au anaumwa, hivyo ni vema kukukumbuka ni nini kinaendelea kwenye maisha yako.

Ni hekima kutambua nini kilitendeka katika maisha yako, kama hutakumbuka Mungu kufanya nini katika maisha yako basi kukua katika Kristo inakuwa ngumu sana. Baada ya pasaka Musa Akawaambia watuwake mambo haya: Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Musa alimwendea Farao akiwa na nguvu ya Mungu, lakini alipoelekea bahari ya Shamu alikuwa na uwepo wa Mungu na palipo na uwepo wa Mungu pana nguvu ya Mungu. Katika uwepo wa Mungu hakuna uchache bali kuna utele lakini hautaweza kuufikia kama haujakua kiroho, kuwepo katika uwepo wa Mungu kunahitaji nidhamu kama hautakumbuka nini kilitokea hataruhusu nguvu yake iende na wewe. Atakupa nguvu zake ili ufukuze mapepo na kuponya wagonjwa lakini si uwepo wake. Mungu anakupa kutumia uwezo ulionao kujenga nyumba, kufukuza mapepo, na kuna vitu ambavyo hutaki kutumia uwezo wako na ndiyo maana Mungu alimwambia Musa gawanya bahari “wakavuka” na walipomaliza adui zao walizama hapo baharini.

Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

Kutoka 15:6

Anazungumzia kuhusu mkono wa Mungu, maana kuna nguvu ya Mungu na mkono wa Mungu. Ukisoma Biblia utabaini kuwa ajabu la kwanza ambalo Musa alifanya ni kuhusu nyoka mpaka pigo la tisa aliamuru Musa, lakini ilipofika pigo la kumi Mungu alifanya mwenyewe lakini ilipofika saa ya kuua alifanya mwenyewe. Katika safari hii ya wokovu hakikisha unapata taarifa za kutosha kuhusu wewe ni nani. Mungu hakutaka wana wa Israeli kuua watu wa Misri kwa sababu hawa Wamisri walikuwa ni wakuu wao, watu ambao waliwalisha chakula, walikuwa wakuu wao. Ndiyo maana Daudi hakutaka kumuua Sauli kwa sababu alikuwa mkuu wao. Ukiona mkuu au kiongozi wako anakutesa usijaribu kumuua hivyo nakushauri ukiona tatizo kwake wewe kimbia tu. Mtu yeyote anayekuwa mkubwa, tambua ameruhusiwa na Mungu. Kiongozi ni kiongozi! Mungu alishawaonya wana Isreli. Hii ni sababu pekee ambayo ilipelekea Mungu asiruhusu wana wa Israeli kuwaua Wamisri. Ukimgusa aliye juu yako humgusi yeye, bali unamgusa Mungu aliye juu yake.

Hatuhitaji kugombana na walioko juu yetu, kama unatamani kutembea na Mungu na kuwa na uwepo wa Mungu sio sifa kubishana na bosi wako. Na wewe kiongozi Mungu akikuinua usiwatese walio chini yako!

Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

Kutoka 15:16

Walikuwa na tabia ya kwenda kuwafuatilia, lakini tunaona hapa sasa akawavusha wa kwake na akawaangaiza adui.

Ni wakati gani hawa watu walinunuliwa? Walinunuliwa walipokuwa wanakula pasaka, kwa tendo la pasaka Musa aliwaambia “Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.

Kutoka 15:17

Siku utakapo kubali kwamba umenunuliwa kwa Damu ya Yesu ndiyo siku ambayo kung’ang’ana kwako kutakoma, je unakubali kwamba umenunuliwa? Kama umenunuliwa lazima utende sawa sawa na mnunuzi (Yesu) ukifanya hivyo atakupa kupanda katika mlima wake na katika urithi wake hivyo unakuwa mrithi, kwa nini unateseka leo? Kwa sababu haujakubali kwamba umenunuliwa. Ukikubali kununuliwa unaingia kwa kutimiza mambo haya matatu: utiifu, uaminifu, kujitoa.

 1. Uaminifu ni Mungu “Mungu ni mwaminifu, hivyo ukiwa unaaminika mbele za Mungu na wanadamu ina maana sasa unamwakilisha Mungu sawasawa”
 2. Utiifu ni Yesu “hivyokatika utii unafanyika mwana wa Mungu”
 3. Kujitoa ni Roho Mtakatifu “hii ni kazi ya roho, kujitoa unapokuwa unajitoa unakuwa unamvutia Roho Mtakatifu”

Hivyo uaminifu wako unaisababisha mbingu ikuamini, hivyo unaweza kupewa kuwa na vingi hata ukuu. Utii utakusababisha ustawi ili ule na kuishi vizuri. Na kujitoa kunakusababisha uwe katika uwepo wa Mungu, uweze kubeba nguvu zake na uwepo wake, na hapo ndipo unaruhusiwa kumwakilisha, unaruhusiwa kubeba karama za roho na unaruhusiwa kuitwa mafuta.

Unapoishia kujitoa unakuwa ni mbegu na sasa unaweza kupandwa! Na sasa unaweza kuitwa heri mtu yule maana umepandwa na sasa unakuwa na urithi wako. Unajikuta si wewe tena.

Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? 25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko.

Kutoka 15:23-25

Safari hii ni safari ya kutoka au safari ya Ukombozi, yaani kutoka kwenye mateso. Utakuwa unakombolewa hatua kwa hatua na siku ukifika sasa utasema nimeipata. Kwa nini watu ambao walikuwa wakimsifu Mungu walianza kunung’unika? Watu walewale walioshangilia kuwa wameanza safari ndiyo walioanza kulalamika, sababu ya kulalamika kwao ilikuwa kwa sababu walisafiri siku tatu bila kukuta maji. Mungu alikuwa akiwafundisha ni jinsi gani ya kupambana na maisha. Kimsingi alitaka wamyumaini Mungu kwa kila kitu. Na utaona hata walipoyakuta maji yalikuwa ni machungu na akawaonesha kwamba kwenye kila tatizo lililoko hapo ulipo lina jawabu hapo hapo ulipo. Ni kweli jambo hilo linaweza kuwa gumu lakini linawezekana. Kilichotokea ni kwamba Mungu aliwapa mti wakanywa maji.

Kilichofuata aliwakemea, kwa sababu walikuwa wanalalamika badala ya kumwambia Musa kuwa tuna kiu ya kunywa maji. Mungu hakuyaponya maji bali Musa ndiye aliyeyaponya, unahitaji kuwa na Mungu ili akujuze jinsi ya kufanya.

Majibu yako hayapo Arusha, Mwanza, Sengerema wala Zanzibar bali majibu yako yapo hapo pembeni yako. Baada ya kuwapa maji na kunywa kilichofuata kilikuwa ni kukemewa, kwa nini awakemee? Kwa sababu walimuona Mungu tangu mwanzo lakini kwa nini walikuwa wanamtilia mashaka? Wangemwambia Musa tunakiu na si kuanza kunung’unika.

Likitokea jambo gumu katika maisha yako acha kunung’unika uliza kwa upole kwani majibu yake yapo. Hapa wamama mnapaswa kuponyeka, unapoona jambo haulielewi kwa mumeo uliza ujibiwe na si kuanza kunung’unika kwa maana mengine ni hisia zako, unahisi hakupendi lakini sio kweli, sasa badala ya kuanzisha ugomvi muulize kwa upole utajibiwa.

akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

Kutoka 15:26

Kama tutaisikia sauti ya Bwana hata kugombana hatutagombana kamwe. Mungu hapendi uone tatizo la Mwenzako, bali atapenda kwanza ujione matatizo yako. Hapa kuna mambo ya msingi matatu anayoyaelezea!

 • Magonjwa: ndiyo yanaangamiza zaidi ya kitu chochote.
 • Kuna mambo ambayo yanahusu mambo wasiomjua Mungu nakuna mambo ambayo yanahusu wanaojua Mungu. Hivyo kuna mambo ambayo halitakiwi yawasumbue watu wamjuao Mungu. Sasa inashangaza kuona watu wanaomjua Mungu wanasumbuliwa na mambo ambayo yanatakiwa kuwasubua wasiomjua Mungu.
 • Mungu anatuonesha kwamba yanayoendelea kwa wasiomjua Mungu na wamjuao Mungu ni yeye anayeyaruhusu. Tunajifunza kwamba Mungu yuko juu ya yote! Yaani alimpa Musa nguvu na Akampa Farao wimbo!

Mungu amesema hivi, kama utasikia yale yaliyokuwa yanakutesa yataondoka kwako.

MAOMBI:

 1. Ee Baba wa Mbinguni, naoba unipe neema ya kusikia na kuzingatia kile ninachosikia.
 2. Baba kwa Jina la Yesu Kristo naomba unifikishe salama mwisho wa safari hii. Nakupenda baba yangu!

KUTAMKA NI KANUNI YA UUMBAJI

Maisha yanaweza kubadilishwa na kanuni ya uumbaji pekee, sababu kubwa ni kwmba Mungu amekupa nguvu ndani yako wa kutamka jambo na likawa halisi, jambo la msingi ni kuamini. Kama uko ndani ya Yesu Kristo haya mamb ni mepesi mno.

Naomba utambue kuwa maombi yako yanawafanya malaika waweze kufanya kazi lakini ukiri wako unaomfanya Roho Mtakatatifu afanye kazi kwa niaba yako. Maneno unayoyatamka au kutangaza ni ndiyo malighafi ya Roho Mtakatifu kukutimizia matarajio yako, maono yako na ndoto zako.

Katika uumbaji wa dunia hii hakuna kilichotokea mpaka Mungu alipotamka, licha ya kwamba Roho Mtakatifu alikuwepo palepale alitulia juu ya maji.

Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. 3 Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.”

Mwanzo 1:2-3

Roho Mtakatifu alitiza matamanio au matarajio ya Mungu. Nikukumbushe tu pale katika bonde la mifupa mikavu hakuna ambacho kingetokea kama kama nabii Ezekieli asingetamka neno.

Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana.”

Ezekieli 37:4

Hoja ya msingi hapo ni kwamba Ezekieli aliambiwa “uiambie”. Tunaona kanuni ile ile ambayo Mungu aliitumia kutamka juu ya uumbaji wa dunia ndiyo ambayo ilitumika kuifanya mifupa mikavu ikaanza kusogeleana..

akaendelea kuiambia, mishipa ikatokeza,

akaendelea kuaimbia nyama zikatokeza,

akaendela kutamka juu ya upepo na pumzi ikaijia ile mifupa.

Utabaini kwamba tumezoea kulalamika sana kuwa maisha magumu, au vyumavimekaza. Kinachotakiwa kutumika hapo ni kutumia kanuni ya uumbaji kutengeneza hali mpya. Na hili halitakaa litokee mpaka umeamua kutangaza unachotamani kukiona.

Inawezekana unatamani kuona Uponyaji, tangaza.

Inawezekana unatamani kuona ndoa nzuri, tangaza.

Inawezekana unatamani kuona amani moyoni mwako, tangaza.

Inawezekana unatamani kupata ajira au kupanda cheo, tangaza.

Inawezekana wewe unatamani kuishi maisha marefu, tangaza.

Inawezekana kiu yako ni kupata mtaji, tangaza,

Inawezekana una hofu ya kufa kwa korona, tangaza.

Katika Ulimwengu wa roho, viumbe vina akili, vinasikia. Vinao uwezo wa kuwasiliana na kuitikia unachotamka au kutangaza. Kila kitu kinaumbwa kwa neno, na vinaitika kwa neno lililotamkwa na Mungu au watu (Yohana 1:1-5).

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.  4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza”.

Yohana 1:1-5.

Usikate tamaa! Umba jambo lolote ambalo unatamani Mungu afanye. Wewe tangaza kwa sauti, ukijua kabisa mbingu zinasikia na kuzimu kunasikia kuwa kuna mtu sasa ameolewa na ameamua kuchukua nafasi yake.

Na huo ndiyo mwisho wa matatizo yako!

Ubarikiwe Daima!

KWA NINI WAKRISTO WENGI HAWAONI NGUVU ZA MUNGU?

Wakristo wengi wanaufahamu msalaba wa YESU, unaowapa msamaha wa dhambi. Lakini wengi hawajawahi kuchukua hatua ya UFUFUO wa Yesu Kristo. Maana Msalaba ni Upendo wa Mungu na Ufufuo ni nguvu ya Mungu.

Tunapochukua hatua ya kuhamia katika msamaha wa dhambi na nguvu ya ufufuo wa Yesu Kristo. Ndipo anapodhirisha ushindi wake katika maisha yetu na ya wengine’.

Tunahitaji vyote (upendo na nguvu). Bila Upendo Nguvu zake zitatuharibu au tutaharibu wengine. Na bila ya nguvu Upendo wake hauna kazi. Wakristo wengi wana upendo kwa Mungu lakini hawana nguvu ya kushinda magonjwa, nguvu za giza, uovu, na nguvu za kipepo – hujitukuta wakishindwa vita.

BAADHI YA CHANGAMOTO ZA MTUMISHI

Mtumishi wa Mungu lazima awe makini sana na baadhi ya vitu, ili mwishowe asije akaangukia mikononi mwa ibilisi. Changamoto kubwa ni hizi zifuatazo: – 

 1. Nguvu
 • Nguvu inaweza kuua

Nguvu inasidia sana kwenye ulinzi. Tunaona 2 Wafalme 1:9-12, ambapo tunaona maaskari waligeuzwa majivu palepale. Hii ndiyo nguvu. Mungu wa Eliya ndiye Mungu wako, ile nguvu bado ipo hata sasa kama ilivyokuwa wakati ule wa Elia. Ukiwa na nguvu ya Mungu unaweza kumshughulikia adui. Nguvu ni nzuri lakini lazima idhibitiwe.

Kama Mungu ataweka nguvu kubwa kwa mtu ambaye hawezi kuitawala, kutatokea uharibifu mwingi sana. Mungu hawezi kuachilia nguvu zake kwa mtu ambaye hawezi kuitumia vizuri. Hebu fikiri mtu kichaa akipewa bomu nini kitatokea? Kama bado una hasira sahau kupata nguvu ya Mungu.

 • Nguvu inaweza kukuharibu

2 Samweli 11:1-27, hapo tunaona nguvu ikimharibu Mfalme Daudi, alipopata cheo akiwa matembezini akaona mke wa mtu akioga, kama mfalme akatoa amri kuwa yule mwanamke apelekwe kwake. Yule mwanamke akapata ujauzito wake na alitumia nguvu zake kupanga mauaji ya mme wa yule mwanamke.

 • Nguvu inaweza kumwangamiza aliye ibeba.

Kwa kuwa nguvu za Mungu zinaweza kupelekea mtu kiburi. Katika Waamuzi 16, tunaona habari za Samsoni. Wazazi wake walimuonya asioe mwanamke ambaye hajaokoka, lakini hakuwasikiliza. Samsoni akaishia kuangamia.

 • Nguvu inaweza kuwa chanzo kikubwa cha majaribu.

Ukisoma Mathayo 3:16-17 na ukilinganisha na Mathayo 4:1-11, utagundua kuwa ghafla Yesu alipobatizwa ubatizo na Roho Mtakatifu ndipo ibilisi akampeleka katika majaribu mazito. Ibilisi alimuomba Yesu kutumia nguvu zake kubadili jiwe liwe mkate. Ibilisi alitaka Yesu atumie zile nguvu kujishibisha. Tambua kuwa ibilisi anaweza kukushawishi utumie nguvu ulizo nazo kujilimbikizia mali. Mungu akikupa kanisa la kuchunga usiligeuze kuwa chanzo chako cha kujipatia chakula. Haimaanishi kuwa ni kosa kanisa kukupa chakula bali nina maanisha wewe zingatia kufanya ya Bwana na Bwana atafanya yanayokuhusu.

 1. Kukosa uzoefu

Uzoefu ni mwalimu bora sana. Kuna faida kubwa sana za kujifunza kutokana na uzoefu wa watumishi waliotutangulia ili ujue namna gani ya kushinda. Maana uzoefu unaweza kujifunza kwa kutazama wengine au kwa kupitia mwenyewe.

Samweli alijifunza kwa Eli. Alitambua kwamba ni kwa sababu watoto wa Eli walikuwa wakicheza na sadaka za Mungu, walikosa nidhamu na kufanya uzinzi na kuchafua nyumba ya Mungu, ilipelekea Mungu kusema katika 1 Samweli 2:30:

Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.”

Samweli akalipata hili somo. Maisha yake yote na watoto wake walijizuia kabisa kuichafua madhabahu ya Mungu (1 Samweli 12:1-5).

Daudi alipata uzoefu kwa mfalme Sauli. Ndiyo maana katika 2 Samweli 6:14-22, alicheza mbele za Bwana kwa uwezo wake wote.

Mfalme Nebukadreza alijifunza kutokana na aliyoyapitia mwenyewe katika Danieli 4, Mungu alimuonya kupitia ndoto. Mungu akamwandalia na mpango wa kutafsiriwa ndoto, lakini akapuuzia onyo. Kwa miaka saba alikula majani kama mnyama ndipo akapata ufahamu na kutambua kuwa mfalme wa kweli ni Mungu.

Kama kuna somo moja kubwa la kujifunza kwa Farao, ni kwamba haiwezekani kupigana na Mungu na ukashinda. Maana Biblia inasema:

“Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.”

Warumi 9:17
 1. Uwezo wako.

Changamoto kubwa hapa ni kwamba Mungu ana vitu vingi sana na hata anapotupa anatoa kwa kadri ya wingi wa utajiri wake, lakini tatizo kubwa ni uwezo wa Mtumishi kuchukua kutoka kwa Mungu.

Zaburi 23:5 inasema:

Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika

Wakati wote Mungu anapotoa, anatoa mpaka mpokeaji anachanganyikiwa (Malaki 3:10, Mithali 3:9-10). Katika Yohana 2:1-11, katika harusi ya Kana, kilichotakiwa ilikuwa ni divai ili sherehe iishe salama. Lakini alitoa zaidi ya walichohitaji na ilikuwa divai bora sana. Mungu anasema endapo utayatenda mapenzi yake atakubariki kiasi kwamba baraka zitakuwa zikikukimbiza na kukupata.

Kama Mungu anajitosheleza kwa nini Mtumishi unakosa upako wa kutosha? Kwa nini unapungukiwa fedha? Kwa nini uko upande wa moto na bado umeoza? Kwa nini uko kwenye ukingo wa mto na bado una kiu?

 • Inawezekana unatamani vitu visivyo, pengine unatamani utajiri. Mithali 23:5 “Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni.” Maana mara nyingi wanaotamani mali hunaswa katika mtego.
 • Pengine unaomba Mungu akupe kutambulika. Yeremia 45:5 inasema “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema Bwana; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.”
 • Pengine unatafuta mamlaka. Mamlaka au nguvu inaua. Katika 2 Mambo ya Nyakati 26 mfalme Uzia alimlingana Bwana na akawa tajiri sana. baadaye akamkosea Mungu na akaangamizwa. Vivyo hivyo kwa Samsoni katika Waamuzi 14:1-3, Samsoni alisisitiza kwamba ataoa mahali ambapo si sahihi, kwa kutumia nguvu zake licha ya maonyo ya wazazi wake.

Una kiu kiasi gani kwa ajili ya mambo ya Mungu? Katika Mathayo 5:6 Biblia inasema:

Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”

Mathayo 5:6

Sababu ya kwa nini huna kitu inawezekana wewe bado ni bahili. Maana mtu bahili atazidi kuusogelea uhitaji daima. Mithali 11:24-25, inathibitisha hili:

Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.”

Mithali 11:24-25

Unachotoa kinaamua upate nini. Luka 6:38 inasema;

Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa

Luka 6:38

Ukuu unategemea sana kiasi gani unatoa na si muhimu sana kwamba una nini. Katika 2 Wafalme 4:8-17, mwanamke Mshunami aliitwa ‘mkuu’ si kwa sababu ya utajiri wake, ila kwa sababu alikuwa mtoaji sana. umewahi kutoa bila kuombwa? Je umewahi kujitoa kuomba kwa ajili ya mkubwa wako bila yeye kukuagiza?

Mwamba wa upako ni huduma ya kujichotea tu. Mungu akiona kwamba una hiari ya kutoa muda wako na nguvu kwa ajili ya wengine, upako utakujilia. Je uko tayari kufa ili wengine waishi? Kama kweli basi tambua Mungu atakuagiza umpelekee vyombo vyako tu ili yeye aweze kuvijaza mpaka vifurike na upako. Kama unatamani kutumia, kubali kutumiwa, ataleta upako kwako.

 1. Kujiongoza.

Hali ya kujiongoza inaanza pale ambapo unaona kama unabanwa, unaanza kuona kama umekua na unazuiliwa kupaa kama utakavyo. Unapoanza kuona hali ya kutofurahia utumishi wa kuwa chini ya mtu unatakiwa kuwa makini sana, inawezekana unataka kuanza kujiongoza.

Mwana mpotevu alikuwa na wazo la kutaka uhuru ili ajiongoze mwenyewe na akaanza kudai urithi wake.

Ole wa watoto waasi; asema Bwana; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi; 2 waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri. 3 Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu.”

Isaya 30:1-3

Baada ya Mwana mpotevu kuupata uhuru alioutaka zikaanza starehe, akaanza kujifurahisha. Akaanza kuishi atakavyo, alienda kwenye starehe kila siku. Lakini ikumbukwe kuwa uhuru ukizidi unasababisha kupoteza na kuharibikiwa. Na ukisha poteza ulichokuwa unajivunia ndipo aibu inakufuata. Unajua kuwa tawi la mti likikatwa toka kwenye shina, kwa kitambo fulani bado linaendelea kuwa majani yenye rangi ya kijani. Hii ni kwa sababu kunakuwa bado kuna virutubisho vimetunzwa kwenye tawi. Lakini vile virutubisho vya chakula vikiisha kinachofuata ni majani kukauka.

Watumishi wengi sana wanaojitafutia uhuru kwa matakwa yao wamejikuta wakiishia katika aibu kubwa baada ya kushindwa katika utumishi wao.

 1. Roho za mazoea.

Roho za mazoea zipo kwenye jamii nyingi na ni rahisi kuua kazi ya Mtumishi. Zinatokana na mwingiliano kati ya mtumishi na anaowaongoza, hali inayowapa nafasi ya kufahamu mambo mengi kuhusu Mtumishi wao. Anavyoweka watu karibu naye wanaingiwa na roho ya mazoea. Hata Bwana Yesu alipokutana na watu wa namna hii, aliwaombea na kuponya wachache tu kutokana na kuwa watu wa dharau.

Yesu Akasema, Amini, nawaambia ya kwamba, hakuna Nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.

Luka 4:24, 28-29

Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika Sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini.”

NGUVU

Mtume Paulo alipotoka jangwani baada ya Mungu kumchukua na kumbadilisha akiwa njiani kuelekea Dameski, aliweza kusema, “… mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu (Wagalatia 1:16)”

Alienda katika miji na kusema “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu”

“nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi. Nilikuwa mwanafunzi wa wanafunzi, nimekuwa Mwalimu wa Walimu. Mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo.”

“Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.”

Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. 5 Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, 6 kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”

Wafilipi 3:4-6.

MAFANIKIO MAPYA YA KIROHO

Lakini mtume Paulo anasema chochote

“Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo.”

Wafilipi 3:7-8

Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu”

1 Wakorintho 2:4

UDHIHIRISHO WA NGUVU

Paulo na washirika wengine wa kanisa la Mungu walisitaajabisha ulimwengu wa kisiasa wa kipindi walichoishi kwa nguvu ya Roho wa Mungu Anayeishi.

Kanisa la Yesu Kristo, lilizaliwa kupitia udhihirisho wa NGUVU ya kitume.

Je, leo tuna nini?

Tuna nadharia nyingi mno.

Tuna theolojia nyingi mno.

Tuna mafundisho mengi mno.

Lakina hatuna udhihirisho wa nguvu za Mungu!

Yesu Kristo anakuja mara ya pili na kanisa litanyakuliwa.

Je, umewahi kufikiri hata kwa dakika moja kwamba kanisa litanyakuliwa likiwa halina nguvu, lina anemia, limedhoofu, limelala, lisilojali hali iliyopo leo?

Kanisa lilinyakuliwa ni Bibi Harusi wa Kristo. Ni zawadi ya pekee atoayo Baba kwa mwanaye wa pekee, Yesu, kwa kazi yake ya Ukombozi aliyoikamilisha hapa dunia, kwa kuacha utukufu mkubwa uliomzunguka kule mbinguni na akachukua ufanano wa mwili wa dhambi, kwa kuvumilia mateso, kukataliwa na maumivu ili tu kwamba ajitoe kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima

Je, unafikiri kuwa Mungu ataridhika kuona alitoa zawadi ya pekee ya Mwanaye Yesu Kristo na kupitia maumivu makubwa kiasi kile na aone Bwana Harusi, anamletea kanisa nyonge kama tulionavyo leo?

Ukweli haiwezekani, lazima jambo fulani lotokee. Lazima tulifanye litokee. Nakutabilia kuwa moja ya mafanikio makubwa ambayo utayapata katika ulimwengu wa roho kwa jinsi ujio wa mara ya pili wa Yesu Kristo unakaribia ni:

Kanisa La Yesu Kristo Litanyakuliwa Likiwa Na Udhihirisho Wa Nguvu Za Mungu Za Ajabu Mno  Na  Roho Mtakatifu Atamwangwa Kuliko Hata Kanisa Lilivyokuwa Linaanza.

Kanisa lilizaliwa katika nguvu. Ilieleweka kabisa kuwa kanisa lina nguvu. Kulikuwa na miale ya moto. Kulikuwa na kunena kwa lugha mpya. Kulikuwa na nguvu. Unaweza kusoma kipande kidogo tu cha Matendo ya Mitume Kuhusu kanisa la kwanza na ukaona jinsi ambavyo hawa watu walitembea katika nguvu za Mungu. Kubwa tena kubwa mno. Watu walijaa nguvu.

Mungu alichukua wanaume na na wanawake wabishi, waoga, wasio na elimu, wasiojulikana, na wengine hata hawakujua hazina za dunia hii, lakini Mungu aliwasha moto wa nguvu za mbinguni ndani yao na wakaweza kuifagilia dunia kwa Yesu.

Hili linafananaje na kile ambacho tunakiona siku za leo?

Ninao ujasiri wa kukuambia kuwa mpaka leo bado sura ya mwisho ya kitabu cha matendo ya  Mitume wa dunia hii bado haijaandikwa na haijafungwa!

Siku moja nilipomaliza tu kuomba usiku wa saa nane, Bwana Yesu alikuja chumbani kwangu, mwili mzima ulizimia ganzi kwa kuona tu ule mwanga wake nakumbuka ilikuw ani Tarehe 27 Julai 2014. Bwana aliponitokea nguvu zote zikaisha na alikuja kuniambia tunifundishe viongozi, sikulala mpaka asubuhina kesho yake sikuweza kuhubiri nilisimulia tukio na kulia tuna watu walifunguliwa sana.

Kazi ya Mungu si kazi ya mtu, hivyo tunahitaji kuwa na vitendea kazi vya mwenye kazi, ambavyo ni Roho Mtakatifu na nguvu za Mungu.

Kwa kadri tunavyozidi kutamani kuwa karibu naye, nguvu, uwepo wake, upako, utukufu ufufuo wa Yesu Kristo na udhihirisho wa Roho Mtakatifu utakuja kwetu katika ulimwengu wa roho na kudhihirka katika ulimwengu wa kawaida (asili). Ukweli tunaenda katika viwango aambavyo macho hayajapata kuona wala masikio hayajawahikusikia, kabla ya unyakuo tutatembea katika viwango vikubwa na vya kushangaza mno.

Dunia nzima itajua kwamba Yesu yu Hai, kwamba ni Mwana wa Mungu,na kwamba alikuja huku duniani kwa kusudi. Wataona nguvu zake zikidhihirika ndaniya watu Wake kwa namna ya ajabu sana.

Yesu alisema;

Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”

Mathayo 24:14.

Tupo katika kipindi cha mpenyo (kufanikiwa), kipindi cha kutoa uthibitisho (ushuhuda) kwanguvu.

Tunaweza, ni lazima, tutafanya, acha kujiwazia huwezi, si wewe bali Mungu ndani yako. Vuka mipaka ya uwezo wako wa kufikiria.

🗣 OMBA:

 1. Omba Mungu mwenye nguvu, uliye Baba yangu nijalie Mtumishi wako, kufikia hatua yakudhihirisha nguvu zako, nina kiu na uwepo wako maishani mwangu, katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

Unaweza kujiunga kwenye group la Goodvine Discipleship School la WHATSAPP kwa kujaza fomu hapa chini:

http://forms.gle/957djapjw8gFLkF36