👤 Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira [🇹🇿]

Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; 14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

Waefeso 4:12-14

Lengo kubwa la mafundisho haya ili tuweze kukamilishwa na kujengwa ili kufika pale Mungu alipotuandalia pasipo kupoteza mwelekeo wa udanganyifu wa ibilisi. Kuna vitu vitakuja kutoka kwa ibilisi na vitakusukuma huku na kule au kuna watu watakuja na ufahamu wao na kwa kupitia neno la Mungu na watakusukuma na wewe kwa sababu hukumbuki Neno linasema nini unajikuta umeingia mahali ambapo hukutakiwa uingie.

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 2 Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

Kutoka 15:1-2

Mungu anapokupa kitu ambacho hukustahili inabidi umsifu mfano kupata mke au mme ni mpango wa Mungu. Tambua kuwa hata kupata mtoto ni mkono wa Mungu – ina maana kuwa sio kwa nguvu zako bali kwa mkono wa Bwana.  Kuna mambo makuu mawili ambayo tunajifunza hapa:

  1. Kujua kipi katika maisha yako ni mkono wa Mungu na kipi ni nguvu ya Mungu.
  2. Baada ya kugundua peleka shukrani au sifa kama ni wimbo au kwa chochote. Kuna vitu vingine ambavyo ni kwa uwezo wako: mfano kuamka asubuhi sio nguvu zako. Wewe ukiamkaasbuhi sio uwezo wako, wengine akiamka asubuhi anakuwa amekufa au anaumwa, hivyo ni vema kukukumbuka ni nini kinaendelea kwenye maisha yako.

Ni hekima kutambua nini kilitendeka katika maisha yako, kama hutakumbuka Mungu kufanya nini katika maisha yako basi kukua katika Kristo inakuwa ngumu sana. Baada ya pasaka Musa Akawaambia watuwake mambo haya: Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Musa alimwendea Farao akiwa na nguvu ya Mungu, lakini alipoelekea bahari ya Shamu alikuwa na uwepo wa Mungu na palipo na uwepo wa Mungu pana nguvu ya Mungu. Katika uwepo wa Mungu hakuna uchache bali kuna utele lakini hautaweza kuufikia kama haujakua kiroho, kuwepo katika uwepo wa Mungu kunahitaji nidhamu kama hautakumbuka nini kilitokea hataruhusu nguvu yake iende na wewe. Atakupa nguvu zake ili ufukuze mapepo na kuponya wagonjwa lakini si uwepo wake. Mungu anakupa kutumia uwezo ulionao kujenga nyumba, kufukuza mapepo, na kuna vitu ambavyo hutaki kutumia uwezo wako na ndiyo maana Mungu alimwambia Musa gawanya bahari “wakavuka” na walipomaliza adui zao walizama hapo baharini.

Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

Kutoka 15:6

Anazungumzia kuhusu mkono wa Mungu, maana kuna nguvu ya Mungu na mkono wa Mungu. Ukisoma Biblia utabaini kuwa ajabu la kwanza ambalo Musa alifanya ni kuhusu nyoka mpaka pigo la tisa aliamuru Musa, lakini ilipofika pigo la kumi Mungu alifanya mwenyewe lakini ilipofika saa ya kuua alifanya mwenyewe. Katika safari hii ya wokovu hakikisha unapata taarifa za kutosha kuhusu wewe ni nani. Mungu hakutaka wana wa Israeli kuua watu wa Misri kwa sababu hawa Wamisri walikuwa ni wakuu wao, watu ambao waliwalisha chakula, walikuwa wakuu wao. Ndiyo maana Daudi hakutaka kumuua Sauli kwa sababu alikuwa mkuu wao. Ukiona mkuu au kiongozi wako anakutesa usijaribu kumuua hivyo nakushauri ukiona tatizo kwake wewe kimbia tu. Mtu yeyote anayekuwa mkubwa, tambua ameruhusiwa na Mungu. Kiongozi ni kiongozi! Mungu alishawaonya wana Isreli. Hii ni sababu pekee ambayo ilipelekea Mungu asiruhusu wana wa Israeli kuwaua Wamisri. Ukimgusa aliye juu yako humgusi yeye, bali unamgusa Mungu aliye juu yake.

Hatuhitaji kugombana na walioko juu yetu, kama unatamani kutembea na Mungu na kuwa na uwepo wa Mungu sio sifa kubishana na bosi wako. Na wewe kiongozi Mungu akikuinua usiwatese walio chini yako!

Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

Kutoka 15:16

Walikuwa na tabia ya kwenda kuwafuatilia, lakini tunaona hapa sasa akawavusha wa kwake na akawaangaiza adui.

Ni wakati gani hawa watu walinunuliwa? Walinunuliwa walipokuwa wanakula pasaka, kwa tendo la pasaka Musa aliwaambia “Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele (Kutoka 12:14)”.

Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.

Kutoka 15:17

Siku utakapo kubali kwamba umenunuliwa kwa Damu ya Yesu ndiyo siku ambayo kung’ang’ana kwako kutakoma, je unakubali kwamba umenunuliwa? Kama umenunuliwa lazima utende sawa sawa na mnunuzi (Yesu) ukifanya hivyo atakupa kupanda katika mlima wake na katika urithi wake hivyo unakuwa mrithi, kwa nini unateseka leo? Kwa sababu haujakubali kwamba umenunuliwa. Ukikubali kununuliwa unaingia kwa kutimiza mambo haya matatu: utiifu, uaminifu, kujitoa.

  1. Uaminifu ni Mungu “Mungu ni mwaminifu, hivyo ukiwa unaaminika mbele za Mungu na wanadamu ina maana sasa unamwakilisha Mungu sawasawa”
  2. Utiifu ni Yesu “hivyokatika utii unafanyika mwana wa Mungu”
  3. Kujitoa ni Roho Mtakatifu “hii ni kazi ya roho, kujitoa unapokuwa unajitoa unakuwa unamvutia Roho Mtakatifu”

Hivyo uaminifu wako unaisababisha mbingu ikuamini, hivyo unaweza kupewa kuwa na vingi hata ukuu. Utii utakusababisha ustawi ili ule na kuishi vizuri. Na kujitoa kunakusababisha uwe katika uwepo wa Mungu, uweze kubeba nguvu zake na uwepo wake, na hapo ndipo unaruhusiwa kumwakilisha, unaruhusiwa kubeba karama za roho na unaruhusiwa kuitwa mafuta.

Unapoishia kujitoa unakuwa ni mbegu na sasa unaweza kupandwa! Na sasa unaweza kuitwa heri mtu yule maana umepandwa na sasa unakuwa na urithi wako. Unajikuta si wewe tena.

Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? 25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko.

Kutoka 15:23-25

Safari hii ni safari ya kutoka au safari ya Ukombozi, yaani kutoka kwenye mateso. Utakuwa unakombolewa hatua kwa hatua na siku ukifika sasa utasema nimeipata. Kwa nini watu ambao walikuwa wakimsifu Mungu walianza kunung’unika? Watu walewale walioshangilia kuwa wameanza safari ndiyo walioanza kulalamika, sababu ya kulalamika kwao ilikuwa kwa sababu walisafiri siku tatu bila kukuta maji. Mungu alikuwa akiwafundisha ni jinsi gani ya kupambana na maisha. Kimsingi alitaka wamyumaini Mungu kwa kila kitu. Na utaona hata walipoyakuta maji yalikuwa ni machungu na akawaonesha kwamba kwenye kila tatizo lililoko hapo ulipo lina jawabu hapo hapo ulipo. Ni kweli jambo hilo linaweza kuwa gumu lakini linawezekana. Kilichotokea ni kwamba Mungu aliwapa mti wakanywa maji.

Kilichofuata aliwakemea, kwa sababu walikuwa wanalalamika badala ya kumwambia Musa kuwa tuna kiu ya kunywa maji. Mungu hakuyaponya maji bali Musa ndiye aliyeyaponya, unahitaji kuwa na Mungu ili akujuze jinsi ya kufanya.

Majibu yako hayapo Arusha, Mwanza, Sengerema wala Zanzibar bali majibu yako yapo hapo pembeni yako. Baada ya kuwapa maji na kunywa kilichofuata kilikuwa ni kukemewa, kwa nini awakemee? Kwa sababu walimuona Mungu tangu mwanzo lakini kwa nini walikuwa wanamtilia mashaka? Wangemwambia Musa tunakiu na si kuanza kunung’unika.

Likitokea jambo gumu katika maisha yako acha kunung’unika uliza kwa upole kwani majibu yake yapo. Hapa wamama mnapaswa kuponyeka, unapoona jambo haulielewi kwa mumeo uliza ujibiwe na si kuanza kunung’unika kwa maana mengine ni hisia zako, unahisi hakupendi lakini sio kweli, sasa badala ya kuanzisha ugomvi muulize kwa upole utajibiwa.

akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

Kutoka 15:26

Kama tutaisikia sauti ya Bwana hata kugombana hatutagombana kamwe. Mungu hapendi uone tatizo la Mwenzako, bali atapenda kwanza ujione matatizo yako. Hapa kuna mambo ya msingi matatu anayoyaelezea!

  • Magonjwa: ndiyo yanaangamiza zaidi ya kitu chochote.
  • Kuna mambo ambayo yanahusu mambo wasiomjua Mungu nakuna mambo ambayo yanahusu wanaojua Mungu. Hivyo kuna mambo ambayo halitakiwi yawasumbue watu wamjuao Mungu. Sasa inashangaza kuona watu wanaomjua Mungu wanasumbuliwa na mambo ambayo yanatakiwa kuwasubua wasiomjua Mungu.
  • Mungu anatuonesha kwamba yanayoendelea kwa wasiomjua Mungu na wamjuao Mungu ni yeye anayeyaruhusu. Tunajifunza kwamba Mungu yuko juu ya yote! Yaani alimpa Musa nguvu na Akampa Farao wimbo!

Mungu amesema hivi, kama utasikia yale yaliyokuwa yanakutesa yataondoka kwako.

MAOMBI:

  1. Ee Baba wa Mbinguni, naoba unipe neema ya kusikia na kuzingatia kile ninachosikia.
  2. Baba kwa Jina la Yesu Kristo naomba unifikishe salama mwisho wa safari hii. Nakupenda baba yangu!

Toa Maoni yako / Leave Your Comment:

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s