Maombi ni mawasiliano yako na Mungu, yanayohitaji mtu jasiri   na mwenye kujitambua.  Hivyo omba kwa kumaanisha.

Bwana Yesu alisema “Tangu siku za Yohana Mbatizaji, ufalme wa Mungu hutekwa na wenye nguvu.”  Unapoomba kwa ujasiri, maana yake una-agiza mbingu ilete au itende kwa kutii agizo la kifalme.  Ni agizo kwa sababu, kile unachoomba kinaenda moja kwa moja kwa malaika mhusika, mfano; kama ni jambo la ndoa linaenda kwa muhusika wa ndoa na vile vile katika masuala ya fedha.

Kukosa ujasiri kunatokana na dhambi; ni kama mtoto aliye kosea anavyoogopa kumuomba mzazi wake mahitaji yake maana anajua amekosea.

Unapoomba unamaanisha unataka kile unachokitaka kutoka kwake maana Mungu ndiye mpaji; hivyo una sehemu yako kwake; omba!

Maombi ya kinyonge yanatokana na dhambi na kutofanya sawasawa.   Hakikisha moyo wako ni safi na hakuna majuto ndani yako; yaani, husikii kuhukumiwa moyoni Neno likinenwa. Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?”  Mwenye moyo safi hasikii hatia wala hajihukumu; maana yote atendayo na yote anenayo hutenda katika kweli ya Mungu. 

“Heri wenye moyo safi maana watamwona Bwana”

Mathayo 5:8

Neno linasema abishaye hufunguliwa, na aombae hupewa.

“Kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? ”

Mathayo 7:7 – 8

“Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.”

Zaburi 2:7-8

Maombi ni kama madai mbele za Mungu.  Unapoenda kumwomba Mungu ujue kuwa anacho na atakupa; hivyo uwe na uhakika.

“Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.”

Isaya 45:11

“Kwa maana, kwa kupitia kwake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa, tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja. Kwa hiyo, ninyi sasa siyo wageni tena wala wapita njia, bali mmekuwa raia halisi pamoja na watu wa Mungu na familia ya Mungu.”

Efeso 2:18 – 19

Maombi ni agizo kwa warithio ule ufalme wa Mungu katika Kristo Yesu.

“Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.”

Mathayo 17:18-21

Kufunga na kuomba ni sehemu ya unyenyekevu wako kwa Mungu; kunako pelekea kupata maelekezo toka kwake. Ili kufikia mahali pa kufanya kama Bwana Yesu, inatupasa kujishusha, kunyenyekea na kutii kwa Mungu.  Kuhamisha mlima sio kitu chepesi bali inawezekana kwa imani.

Mfano: Tabia ya unyenyekevu na upole ya Musa; pamoja na kufunga na kuomba; ilimpelekea kufikia kiwango cha juu sana cha Imani hata kuweza kuamuru ardhi kufunguka na ikafunguka.

“Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni”.

Nehemia 1:4

Namna mbalimbali za Kuongea na Mungu

  1. Kulia na kuomboleza: Kuomboleza ni njia ya kuongea na Mungu ili kumfanya aone huruma. Tumia njia hii kutaka rehema za Mungu endapo unajua kosa lako; la mtu au la kundi (familia, ukoo, jamii fulani, ofisi, taasisi au Taifa). Kwamba lile tukio ni halali yao au ni halali yako kulipata. Ni kwa yale mambo ambayo unajua kabisa ni haki kutendewa. 2 Nyakati 7:14“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

Mfano: Ukiona kuna misiba, mauaji, laana, tatizo la kiukoo la watu kufa mapema, mfano wengine hawavuki hata miaka 70 au 60 , au aina fulani ya magonjwa inaweza kuwa kansa; unatakiwa kulia na kuomboleza mbele za Mungu ili aweze kuondoa hizo laana.

  1. Kufunga: Unafunga siku kadha wa kadha kwa kutulia pasipo kupeleka hoja yoyote kwa Bwana, ili kumfanya Mungu aone kwamba unamsubiri YEYE; hasa pale unapoona unapitia maumivu na vitu haviendi.  Mfano. Unataka kuolewa na hakuna mchumba anayejitokeza; biashara haziendi; ufukara mwingi na makandamizo ya wakuu wa giza. Kitendo cha kufunga unamwambia Mungu kwamba yasiendelee hayo; maana ukiangalia hayo yanayokupata yana uhalali.
  1. Kuomba: Hii ni njia ambayo unatamka maneno ya hitaji lako, ukimaanisha kwamba unataka usaidizi wake. Unaomba iwapo  mahusiano yako na YEYE ni mazuri. Mathayo 7:9-10 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?  Au akiomba samaki, atampa nyoka?” Hii ni kwa ajili ya Watoto maana wana uhusiano mzuri na Baba yao. Usifanye maombi kama huna mahusiano mazuri na Mungu. Aombaye hupewa; maana maombi ni kwa ajili ya watoto ambao wana kibali.
  1. Sifa: Kumuonesha kwamba YEYE anaweza na ana nguvu, ili aweze kuonesha nguvu zake. Hii ni kwa ajili ya watumishi wake wanaomtumikia, kama ilivyoandikwa; kusifu kunawapasa wanyoofu wa moyo, waliopata neema ya Mungu ndani yao.

Zaburi 33:1 “Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.”  Unafanya hivi unapoona umezingirwa na adui, masumbufu na kuingiliwa katika maisha yako mara kwa mara. Ukiona hayo pale ulipo anza sifa, ili ajitokeze kama mwanaume wa wanaume. Lengo la sifa ni kumfanya ajisikie fahari kwamba Yeye ndiye anaye tegemewa.

  1. Matoleo: Lengo la matoleo ni kumuonesha Mungu kwamba unahitaji ulinzi wake na huduma yake. Hii inatakiwa kwa wale ambao wanateseka na maradhi na magonjwa, wezi, watu wanaowadhurumu, kuibiwa kwenye biashara, kuibiwa mke au mme, ajali, kukosa heshima katika jamii au familia. Toa sadaka utaona ulinzi wake. Mfano Eliya alifanya maombi na kutoa matoleo yake, yaani dhabihu. Kwa lugha nyingine, unapotoa matoleo unamwambia Mungu afanye kwa niaba yako; na ya kwamba unamtegemea.
  1. Shukrani: Inaweza kuwa ya maneno, matoleo au sifa, lakini kwa lengo la kushukuru. Hii inamuonesha kwamba unataka awe mpaji au mfadhili wako. Kwa lugha nyingine unataka Yeye awe hazina yako. Unafanya unapoona uhitaji ni mkubwa na unataka kufanya mambo makubwa. Mfano Unataka kujenga, Yeye anakuwa mfadhili. Utashangaa Mungu anainua watu walete kwako.  Isaya 43:6 “Nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia”
  1. Kucheza: Unapocheza mbele za Mungu, unafanya akupe zawadi; hii ni pamoja na kupewa milki zako, hata milki za maadui zako. Jifunze kucheza mbele zake kwa furaha ili akupe zawadi. Hili unalifanya ukiona huna utoshelevu wa mahitaji yako.  Wana wa Israeli waliimba na kucheza wakati wa vita, wakaokota nyara; wakiongozwa na Mfalme Yehoshafati.
  1. Kuwahi mahala pa Ibada

Swala la kuwahi na kuchelewa mahali pa ibada ni kipimo cha utii na unyenyekevu wako.  Katika yote haya unayofundishwa, inategemea sana utii na unyenyekevu wako kama kipimo mbele za Mungu. Mungu anaangalia sana unavyompa heshima, nafasi na jinsi unavyozingatia majira na nyakati. Ni vyema kuwa mahala pa ibada mapema kabla ibada kuanza ili uweze kujiandaa vema.

Toa Maoni yako / Leave Your Comment:

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s