Taifa letu linapitia changamoto nyingi, lakini wakati huu changamoto kubwa ni janga la ugonjwa wa korona (COVID-19) ambao umesababisha shule na vyuo vyote kufunga, ibada kuendeshwa kwa utaratibu mpya ambao unataka ukaaji wa kuanzia mita moja na zaidi kati ya mtu na mtu, lakini pia mikusanyiko yote ya watu imezuiliwa ikiwemo ya kidini, kisiasa, kijamii na hata harusi hazina sherehe tena. Tunaona kuanzia nyumbani mpaka madukani, kwenye stendi za mabasi, maeneo ya ofisini, ibadani lazima unawe kwa vitakasa mikono (sanitizers) au vitakasa mwili. Si hivyo tu, bali pia mipaka imefungwa na safari zote za ndege pia zimesimamishwa kujikinga na hili janga. Mpaka sasa tumeshuhudia idadi ya wagonjwa ikiongezeka siku kwa siku na waliopona wapo wachache na waliokufa pia wapo, uchumi wa taifa kwa namna moja au nyingine unatingishika kwa sababu ya kufunga safari za ndege, watu wengi kutosafiri kwa mabasi na hata elimu pia imeathiriwa hasa vijana wetu walio na mitihani kama darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na sita. Pia wanchuo ambao wangehitimu mwaka huu ratiba inabadirika na kuathiri mambo mengi mno.

Ni lazima tumuombe Mungu aweze kutushindia hii vita, tutashinda. Neno la Mungu linasema:

Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

Zaburi 33:12

Watu tunaomwabudu Mungu na kutangaza kuwa ni Bwana wetu tutapata baraka zake na ushidndi wa kila namna hata kama kuna magumu sana lakini kwa Mungu yanawezekana. Jambo kubwa la kumshuru Mungu sana ni kwamba Rais John Pombe Magufuli ana hofu ya Mungu na tangu mwanzo wa janga hili amekuwa akitamka wazi kuwa:

 Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” 

Mhe. Rais John Pombe Magufuli

Kwa maneno hayo tunarudi kwenye uzuri wa Mungu wetu aliyesema:

ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.

2 MAMBO YA NYAKATI 7:14-15

Hautwezi kuyapuuza maneno haya ambayo Mungu amenena maana tukitekeleza atasikia na Mungu akisema nitasikia ana maana kwamba nitatenda sawasawa na maombi yao. Kuna mifano isiyohesabika ambayo tunaona kiongozi wa nchi aliitisha maombi ya kitaifa wakiwa katika hali mbaya sana, na Mungu akabadilisha mambo ndani ya muda mfupi. Abraham Lincoln aliwahi kuitisha maombi ya kufunga na kuomba ili kutubu dhambi na uovu dhidi ya utumwa na kiburi cha taifa la Marekani na Mungu akatenda baada ya wao kutubu, ndani ya siku mbili baada ya maombi vita vya wenyewe kwa wenyewe vikakoma na umoja wao ukaonekana tena. Taifa likiamua kuomba Mungu hachelewi kujibu.

kwa nini lazima tufungE na kuomba kitaifa?

Zipo sababu nyingi ambazo hatuwezi kuzilezea kwa utoshelevu, baadhi tu ni kwamba:

 1. Ni lazima tutambue kuwa kufunga kunaondoa nguvu na maneno mengi, unaishiwa nguvu na kuwa mlegevu na kusababisha unyenyekevu wa hali ya juu kwa Mungu na watu pia. Watanzania tunau usemao adui mwombee njaa! maana ikimuuma lazima atanyenyekea na hataweza kupambana tena.
 2. Kwa sababu mfumo mpya wa maisha ya kukaa mbali hapa kwetu Tanzania hauwezekani kutekelezeka kwa asilimia mia, mfano: tunawezaje kuvaa mask kila siku, tunawezaje kukaa mbali na muuzaji huko sokoni, tunawezaje kumudu kujenga madarasa ya kuwafanya wanafunzi wake mita moja au mbili darasani kwa uchumi tulionao sasa?
 3. Tunafunga ili kusamehewa na kupatanishwa na Mungu wetu kwa maana hata Yesu hakuwa na dhambi hata moja lakini alifunga ili kutupatanisha sisi na Mungu. Itakuwa vema sana kama kila Mtanzania atafunga kwa sababu ya kubeba mzigo wa taifa zima na Mungu atatupatanisha naye kupitia Mwanaye -Yesu Kristo. Maana kukiri na kufunga kunaondoa uadui kati yetu na Mungu.

Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; 19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.

2 Wakorintho 5:18
 1. Tunafunga na kuomba ili kuomba toba au rehema, na Mungu anataka sisi tutubu kwa niaba ya wenzetu ambao hawajui namna ya kutubu ili kwamba baraka na neema zake ziweze kumiminwa kwetu. Mungu anasema hivi kwa taifa lenye uovu:

Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo. 17 Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza. 18 Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao. 19 Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa.

Yeremia 6:16-19

Huu ni unabii kwa kila taifa au nchi inayomsahau Mungu na njia zake. Natambua kuwa Tanzania tupo watu ambao hatujamsahau Mungu wetu, lakini baadhi ya Watanzania wamemsahau kabisa. Na Mungu anataka atutumie sisi kusababisha msamaha wake na wengine waliokuwa wamemsahau waweze kumrudia kabla hatujamuomba aponye nchi yetu. Mungu anatungalia sana sisi tulioitwa kwa jina lake tunyenyenekee ili aponye nchi yetu. Ikiponyeka nchi kila mmoja ndani ya nchi anakuwa na amani tele.

toba ni nini?

Mungu wetu anataka tuweze kujitoa kwa nafasi zetu. Maombi yetu ni kujitoa kwa muda na kuacha mambo mengine. kufunga ni kujitoa kwa kuacha raha na kujikana. Toba ni sadaka ya kiburi na kujihudumia mwenyewe. Na kutoa ni sadaka ya kitu tulicho nacho. Sasa tunapoamua kufunga na kutubu hakika tutauoa mkono wa Mungu wetu.

Tunawezaje kulifanya taifa zima liingie kwenye maombi ya pamoja? Ukweli haiwezekani kwa sababu wapo wataokuwa wanabeza na kupuzia kwa kuwa hawana imani kwa Mungu. Lakini tusiogope juu ya hilo kwa sababu wale waaminio tu ndiyo tunaotakiwa kuungana na kuomba kwa ajili ya nchi yetu. Na si lazima tukusanyike pamoja au kwenye chumba kimoja ila tu cha msingi ni kwamba tunaomba kwa umoja – nia moja, nguvu ya Mungu itatujilia.

maombi ya leo siku ya tano

 1. Baba Mungu, kwa jina la Yesu tunakushukuru sana kwa sababu siku ya leo Watanzania wengi wameingia kwenye maombi kwa ajili ya taifa letu la Tanzania. Natambua kuwa leo kuna baraka nyingi sana ambazo tunamiminiwa toka kwako kwa sababu ya wakwambuo na waombao kwako. Asante maana tunajua taifa hili ulilianzisha kwa maombi ya waliotutangulia wakikuamini wewe.
 2. Baba, kwa jina la Yesu, naomba usiwepo ouvu ambao utaliangusha taifa letu, na hakuna tauni (COVID-19) ambayo itatufanya tupoteze mwelekeo. Tusamehe na utupe nguvu ya kuto-ogopa maana tunajua wewe unachukua nafasi ya uponyaji na usalama wetu. Tuponye wakati huu wa masumbuko, tupe maisha marefu na utuoneshe wokovu wako. Utuokoe kwenye mtego wa mwindaji (shetani).
 3. Baba, kwa Jina la Yesu tunakushuru kwa ajili ya waaminio walio katika taifa letu ambao wanakuabudu na kukutumia wewe. Asante sana kwa maombi yao mengi juu ya taifa letu na majibu uliyoayajibu. Tuumbie mioyo ya toba tunaposogea na kunyenyekea mbele zako. Kama taifa tunaomba utusamehe sana kwa kiburi chetu na kukosa imani kwako. Fungua macho yetu tukuone wewe na ukweli wako kwa kadri tunavyoutafuta uso wako.
 4. Baba, kwa jina la Yesu naomba ushushe nguvu ya uponyaji kwa kila aina ya maumivu na magonjwa yaliyolipuka katika taifa letu. Tunajua kwa kadri tunavyokuomba unajibu. Nakuomba siku ya leo mimina Roho yako ya uponyaji kwenye kila mkoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji/mitaa, vitongoji na familia zote – iwe miji, mjini, vijijini, mashuleni, ofisi za serikali, ikulu, maeneo ya biashara, na makanisani katika nchi hii.
 5. Baba, kwa Jina la Yesu tunakuomba ujifunue mwenyewe kila mahali ili watu wakuone na wajue uweza wako. Tunaomba ulete msaada wako ambao unakupa wewe heshima na utukufu.

NYIMBO

 1. POKEA SIFA BWANA
 2. WATOTO WAKO TUMESANYIKA BABA
 3. BABA, SISI TUNAKUABUDU
 4. EE YESU, TWAINUA MACHO YETU
 5. BABA, TWASEMA – ASANTE

Toa Maoni yako / Leave Your Comment:

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s